AR-RAHEEQ AL-MAKHTUM
Baada ya kufariki kwa Abu Twalib, kwa kiasi cha miezi miwili au mitatu (na hapa pana kauli mbili zinazotofautiana) alifariki dunia mama wa waumini Bi Khadija Al-Kubra (Radhi za Allah ziwe juu yake). Alifariki mnamo mwezi wa Ramadhani, mwaka wa kumi wa Utume, akiwa na umri wa miaka sitini na tano na Mtumbe wa Mwenyezi Mungu (ﷺ) akiwa na umri wa miaka khamsini.
Kwa hakika Bi Khadija (Radhi za Allahziwe juu yake) alikuwa ni moja kati ya neema za Mwenyezi Mungu Zilizotukufu kwa Mtume wake (ﷺ). Naye aliishi na Mtume (ﷺ) kwa wema, muda mrefu. Akimhurumia wakati wa kukerwa kwake, akimsaidia katika nyakati zake za matatizo na alimsaidia pia katika kuufikisha ujumbe wake. Alishirikiana naye katika gharama za jihadi yenye uchungu na alimliwaza kwa nafsi yake na mali zake. Mtume wa Mwenyezi Mungu (ﷺ) alisema;
قد آمَنَتْ بي إذ كفَرَ بي الناسُ، وصدَّقَتْني إذ كذَّبَني الناسُ، وواسَتْني بمالِها إذ حرَمَني الناسُ، ورزَقَني اللهُ عزَّ وجلَّ ولَدَها إذ حرَمَني أولادَ النِّساءِ
[ Aliniamini wakati watu waliponikufuru, alinisadikisha wakati watu waliponikadhibisha, alinishirkisha katika mali yake wakati watu waliponinyima na Mwenyezi Mungu Ameniruzuku mimi watoto kutoka kwake, na Hakunipa kutoka kwa asiyekuwa yeye ] (1)
Imepokewa katika hadithi sahihi kutoka kwa Abu Huraira (Radhi za Allah ziwe juu yake) kuwa alisema: Jibril (Alayhi salaam) alimshukia Mtume wa Mwenyezi Mungu (ﷺ) na akamueleza,
يا رسولَ اللهِ ! هذهِ خَديجةُ قد أَتَتْكَ معها إناءٌ فيهِ إدامٌ أو طعامٌ أو شَرابٌ ، فإذا هيَ قد أَتَتْكَ ، فاقرَأ علَيها السَّلامَ مِن ربِّها و مِنِّي ، و بشِّرْها ببَيتٍ في الجنَّةِ مِن قصَبٍ ، لا صَخبَ فيها و لا نَصبَ
[ Ewe Mtume wa Allah huyu Khadija amekuja akiwa na chombo ambacho ndani yake mna kitoweo, au chakula au kinywaji, atakapokujia mtolee salamu kutoka kwa Mala Wake, na mbashirie kasri ya vito huko peponi, hamtakuwa na makelele ndani yake wala taabu yoyote ] (2)
Huzuni juu ya Huzuni:
Matukio haya yenye uchungu yalimtokea Mtume wa Mwenyezi Mungu (ﷺ) katika kipindi cha masiku machache, hisia za huzuni na machungu yakawa yametawala moyo wake Baada ya hapo havikuacha kumuandama vituko kutoka kwa jamaa zake, kwani wao walikuwa wanamfanyia jeuri. Baada ya kufariki kwa Abu Twalib walianza maudhi na mateso, mambo hayo yalimzidishia huzuni juu ya huzuni kiasi cha kuwakatia tamaa.
Aliamua kuondoka na kuelekea Twaif, kwa matarajio kuwa watu wa huko wangeitikia wito wake au wangemuhifadhi na kumnusuru dhidi ya jamaa zake. Hakumpata Twaif aliyekuwa tayari katika hayo; bali hali ilikuwa ni kinyume kabisa na matarajio yake, kero na maudhi ilikuwa ni kubwa sana kuliko ile aliyoipata kutoka kwa jamaa zake.
Kama ambavyo uovu wa watu wa Makka ulivyozidi kwa Mtume (ﷺ) ndivyo ulivyozidi kwa Masahaba zake. Mpaka hatua ya kukimbia rafiki yake Abubakar Al-Siddiq (Radhi za Allah ziwe juu yake). Kwa lengo la kuihama Makka, alitoka mpaka akafika mahali paitwapo Birak Al-Ghimad akiwa na makusudio ya kuelekea Ethiopia, Ibn Ad-Daghna ndiye aliyemrudisha katika dhamana yake.
Ibn Ishaq amesema kuwa, ”Wakati alipofariki Abu Twalib, Mtume wa Mwenyezi Mungu (ﷺ) na Masahaba zake walipata maudhi na mateso kutoka kwa Makuraishi ambayo hawakuwahi kuyapata wakati wa uhai wake. Inasemwa kuwa, siku moja mjinga mmoja, miongoni mwa wajinga wa Kikureishi, alimzuia na kumwagia Mtume (ﷺ) kichwani mwake mchanga. Mtume (ﷺ) alirudi nyumbani kwake akiwa na mchanga kichwani mwake, mmoja kati ya mabinti zake alisimama akawa anauosha mchanga huo na huku akilia, wakati huo Mtume wa Mwenyezi Mungu (ﷺ) akimliwaza kwa kumwambia:
لَا تَبْكِي يَا بُنَيَّةِ، فَإِنَّ اللَّهَ مَانِعٌ أَبَاكَ
[ Usilie ewe binti yangu, hakika Mwenyezi Mungu Atamlinda baba yako.]
Na akawa akimueleza kuwa kabla hapo:
مَا نَالَتْ مِنِّي قُرَيْشٌ شَيْئًا أَكْرَهُهُ، حَتَّى مَاتَ أَبُو طَالِبٍ
[ Makuraishi hawakuthubutu kumfanyia kitu ambacho nikikichukia mpaka alipofariki Abu Twalib.] (3)
Kwa sababu ya kuandamana kwa matukio yenye machungu katika mwaka huu, Mtume (ﷺ) aliuita mwaka huu, ’Mwaka wa huzuni’ na kwa jina hili umekuwa unajulikana katika historia.
Kumwoa Sauda (Radhi za Allah ziwe juu yake)
Mnamo mwezi wa Shawwal katika mwaka wa kumi wa Utume, Mtume (ﷺ) alimwoa Sauda binti Zam’a. Huyu alikuwa ni mmoja miongoni mwa Wale ambaio walisilimu zamani na kuhama katika ile Hijra ya pili kuelekea Uhabeshi, Mume wake alikuwa ni As-Sakran bin Amri, aliyekuwa amesilimu na kuhama pamoja naye, akafariki Uhabeshi au baada ya kurejea Makka. Alipomaliza Eda yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (ﷺ) alimposa na kumwoa. Huyu ndiye aliyekuwa mwanamke wa kwanza aliyemwoa baada ya kufariki kwa mke wake Khadija (Radhi za Allah ziwe juu yake), na baada ya miaka kadhaa kupita zamu yake alimpa Bibi Aisha (Radhi za Allah ziwe juu yao ). (4)