0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

DKT. JERALD F. DIRKS

DKT. JERALD F. DIRKS

“Kwa kutumia mafundisho na elimu ya seminari, nilielewa jinsi gani Biblia ilivyochafuliwa (nilijua wakati, mahali na sababu ya kubadilisha sehemu hizo), sikuwa ni mwenye kuamini tena imani yoyote ya utatu wa Mungu, na sikuwa na imani yoyote kuhusu uwana wa Mungu wa Yesu, amani iwe juu yake. Kwa kifupi, baada ya kupata imani ya kweli ya Mwenyezi Mungu, nimekuwa ni mwenye kuamini Mungu mmoja kama walivyo ndugu zangu Waislamu.”

Dkt. Jerald F. Dirks

Alizaliwa katika familia ya Kikristo, akalelewa katika familia hiyo akihudhuria kanisa na mafundisho yake kila jumapili wakati alivyokuwa mtoto. Alihitimu katika shule nzuri ya seminari na kuteuliwa kuwa mchungaji katika dhehebu kubwa la Kiprotestanti. Baada ya kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Harvard mwaka 1971, Dkt. Jerald aliingia kuendelea kusoma katika Kitengo cha Dini cha Harvard (Harvard Divinity School), na kuchukua shahada yake ya pili akisomea dini mpaka mwaka 1974. Hapo alikuwa tayari kashateuliwa kuwa kuwa mhubiri na mhudumu wa kanisa (United Methodist Church) mwaka 1972. Vile vile ni mwenye udokta wa kitaalamu katika Saikolojia, shahada aliyopata kutoka Chuo Kikuu cha Denver huko huko Marekani.

Kashachapisha zaidi ya makala 60 akongelea masuala ya Saikolojia ya tiba na zaidi ya makala mia na hamsini kuhusu farasi wa kiarabu (Arabian Horse, wanaosifika kwa kasi kubwa, umbo zuri na uwerevu). Ameshatembea sana Mashariki ya Kati na kukutana sana na jamii za kislamu huko Marekani.

Tunamshukuru kwa elimu yake ya kuhusu Ukristo aliyoitoa kutoka katika ghala yake ya maarifa. Elimu iliyosababisha akatoa kauli iliyowazi kueleweka:

“Kuna jambo lililo kinyume ambalo linawakumba wale wanaodhaniwa ni wenye akili, werevu na wajanja, hawa ni wale wanaotayarishwa kuja kuwa wahubiri wa kikristo wanaotolewa kutoka katika shule bora za kiseminari mathalani wale waliosoma shule ya Kikristo ya Harvard kwa kipindi kile. Jambo lenyewe ni kuwa, yule mseminari anaelekezwa ukweli wote wa kihistoria katika mambo fulani fulani mathalani kuhusu: 1) Uundwaji wa asili wa kanisa lenyewe na vipi likageuzwa kwa kuzingatia shughuli za kisiasa; 2) usomaji wa maandiko asili ya Kibiblia, ambayo mengi yao yako kinyume na yale wafuasi wengi wa Ukristo wanasoma pale wanapotumia Biblia zao za kisasa. Hata hivyo, hayo maandishi ya Biblia za kale, pole pole yanaanza kuwekwa katika toleo mapya ya Biblia; 3) kuzaliwa kwa fikra hizi za Utatu na uwana Mungu wa Yesu, amani iwe juu yake; 4) mafundisho yaliyo nje ya dini ambayo sheria au imani za kikristo zimeyakumbatia; 5) kuwapo kwa makanisa ya zamani na harakati za kikristo ambazo kamwe hazikukubaliana na utatu wa Mungu, na ambazo hazikukubaliana na uungu wa Yesu, amani iwe juu yake na 6) mengineyo (baadhi ya haya matunda ya elimu yangu ya seminari nimeyaweka kwa kirefu katika kitabu changu, The Cross and the Crescent: An Interfaith Dialogue between Christianity and Islam, (Alama ya Msalaba na Ile ya Mwezi: Kitabu Kinachozungumzia Mbadilishano wa Mawazo Baina ya Ukristo na Uislamu, Amana Publications, 2001). Kutokana na hivyo haitashangaza kuona wengi kati ya wahitimu wa seminari hizo wakiaga kuiepuka membari wanayotakiwa waipande kuhubiri yale wanayojua sio ya kweli, na kuamua kuingia katika taaluma nyenginezo (kama ushauri/mshauri wa kulipwa) jambo ambalo limenitokea hadi mimi, kwani nikaamua kwenda kuchukua shahada ya pili na ya tatu ya Saikolojia ya tiba. Niliendelea kujiita Mkristo kwa sababu kuna sehemu nilihitajika kujitambulisha na hata hivyo nilisomea uchungaji kanisani, japokuwa muda wote nilikuwa kazini kwangu kama daktari wa akili. Hata hivyo, elimu ile ya seminari imenifanya niwe makini kuingia imani yoyote itakayofundisha Utatu au uungu wa Yesu, amani iwe juu yake. Tafiti zinaonyesha aghalabu wachungaji kanisani huwa hawaamini haya mafundisho na ububusa mwengine kanisani kuliko wale wafuasi wao. Huwa wanaamini maneno kama “mwana wa Mungu” kisitiari tu, wakati wafuasi wao wanaelewa kiuhalisia kabisa.) ndio baadae nikawa Mkristo wa kusubiri Krismas na Pasaka tu, nikihudhuria kanisa kwa kunusanusa hapa na pale, nikijikaza kisabuni na muda mwengine kung’ata ulimi pale ninaposikia mahubiri ambayo nilikuwa najua si ya kweli.”

Pamoja na yote hayo, Dkt. Jerald alibaki kuwa mtu wa dini na bado aliendelea kijinasibisha na Ukristo. Anaandika:

“Nilijua zaidi Ukristo na sikuwa kama wale wanaokubali, bila kusaili, mafundisho na imani ya kanisa yaliyotungwa na binaadamu, ambayo kwa kiasi kikubwa yamepatikana kutokana na athari za kipagani, washirikina na masuala ya kisiasa ya zama za kale.”

Dkt. Jerald na mkewe wamekuwa kwa kiasi kikubwa wakijihusisha na utafiti wa historia wa farasi wa Kiarabu (Arabian horse). Ili wapate tafsiri ya nyaraka mbali mbali za Kiarabu, tafiti zao zikapelekea wakutane na Wamarekani wa kiarabu ambao walikuwa Waislamu. Dkt. Jerald alijifunza mengi katika tabia za Waislamu hao. Sanjari na hilo, Jerald alivutika sana na jamii za kiislamu ukilinganisha na zile za Kimarekani ambazo zilikuwa zimepotea kimaadili. Aligundua katika jamii zile za kiislamu, ndoa zilikuwa imara, wanandoa walikuwa wakijaliana, na uaminifu, uadilifu, kujitolea na tabia njema vilikuwa vinahamasishwa sana. Aliona kabisa Waislamu wakitumia tabia zao nzuri zenye nidhamu na maadili mazuri kote katika maeneo yao ya kazi na kule katika jamii yao.

Jambo lengine lilisababisha kubadili dini kwa Dkt. Jerald ni kule kutamani kwake kugundua vitu kwani alipendelea kusoma vitabu vya kiislamu. Mathalan, ndani ya mwezi, aliweza kusoma karibu vitabu sita au zaidi kuhusu Uislamu, kikiwemo kimoja kinachoongelea wasifu wa bwana Mtume Muhammad. Pia kashasoma aina tatu tofauti ya tafsiri za Qur’an kwa lugha ya Kiengereza. Jerald alisita kuingia katika Uislamu japokuwa alikuwa na mawazo yaliombatana na Uislamu. Kwa maneno yake mwenyewe tulielewa, yapi aliyoyakuta:

“Kitambulisho cha mtu ambacho ndani yake mtu huyo yumo, ni kiri yenye nguvu katika nafasi yake hapa ulimwenguni. Katika kazi zangu za kitaaluma, nimekuwa nikiitwa kutibu matatizo mbalimbali yanayotokana na kutawaliwa na uraibu (addiction), kuanzia uvutaji sigara, pombe mpaka madawa ya kulevya. Kama tabibu nilijua dawa bora kuepuka kitu ulichozoea ni kukiacha. Hiyo ilikuwa sehemu rahisi katika tiba. Kama alivyosema Mark Twain: “Kuacha sigara ni rahisi, nimeshafanya hivyo mara mia.” Lakini nilijua pia ufunguo mkubwa wa kusaidia kuendelea kujiepusha navyo ni kuishinda saikolojia ya mgonjwa, ambayo kwa kiasi kikubwa ipo katika utambulisho (kujulikana) kwa mgonjwa huyo, yaani mathalani mteja akiwa kashazoeleka kujulikana kuwa ni mvutaji sigara au mlevi. Ile tabia yake aliyoizoea ishakuwa kama kitambulisho kwake. Kubadili kitambulisho hiki ni jambo muhimu kwanza ili kuweza kupatiliza matibabu ya kisaikolojia. Hapa ndipo pagumu sasa. Kubadilisha jambo ulilozoeleka nalo ni vigumu sana kisaikolojia. Mgonjwa huwa mwepesi kurudi kwa yale ya zamani aliyoyazoea kuliko mapya na yasiozoeleka kirahisi kwake.

Katika kazi zangu za kitaaluma, nilikuwa nafahamu hayo niliyoyasema, na nilikuwa nikifanyia kazi kila siku. Cha kushangaza sikuwa tayari kulifanyia kazi suala hilo kwangu mwenyewe, nilishindwa kuitumia nadharia hiyo wakati nasita kubadilisha kitambulisho changu cha udini. Kwa miaka 43 sasa, kitambulisho changu katika dini kimekuwa kimebeba jina la Ukristo, hata kama nimeongeza baadhi ya taaluma zilizo tofauti kwa miaka kadhaa kati ya hiyo. Kuachilia kile kitambulisho haikuwa kazi rahisi. Kusita kwangu kulitaka niendelee kushikilia kitambulisho changu cha dini kilichozoeleka cha kuwa Mkristo ingawa ni Mkristo aliyeamini lile ambalo muislmu anaamini.

Ikafikia hadi mwishoni mwa mwezi Disemba, nikiwa na mke wangu tukijaza fomu za maombi ya pasipoti za Marekani, ili ile safari tuliyopanga kwenda Mashariki ya Kati iwe kweli, nilikumbana na swali moja lililokutaka ueleze msimamo wako wa kidini. Wala sikusita na sikufikiria kwani moja kwa moja nilikijaza kile cha mwanzo kilichozoeleka; “Mkristo.” Na bado nilijisikia sawa tu kwa kujaza vile.

Lakini, faraja ile iliharibiwa pale mke wangu aliponiuliza vipi nimejibu swali kuhusu dini katika fomu zile. Nilimjibu kuwa “Mkristo” huku nikicheka kwa sauti. Moja ya msaada wa msomi aitwae Freud katika kuelewa Saikolojia ya mwanadamu ni kugundua kucheka kwa sauti kama moja ya dalili ya kuondoa hofu na hangaiko mwilini mwako. Hata nadharia za Freud katika masuala ya kisaikolojia ziwe za uongo vipi! lakini katika suala hilo la kucheka kwangu halikuwa na shaka. Sasa basi kucheka nishacheka! Cha kujiuliza ni jambo gani lililokuwa likinisuta moyoni mwangu na nikahitaji kulitoa kwa kicheko kile?!

Kwa haraka nikamgeukia mke wangu na kukiri kwa kumtoa wasiwasi kuwa kweli nimeandika Mkristo na sio Muislamu. Yeye akanijibu kuwa alitaka kujua tu kama nimeandika Mkristo, Mprotestanti au Mmethodisti. Kitaaluma yangu, nilijua fika kuwa mtu huwa hajitetei kutoka katika shutuma ambayo haijafanywa bado. (kwa mfano wa kitaalamu, ikatokea mtu akaanza kujishtukia kwa kubwatuka, “Sijakasirika!” iwapo mtu anaeongea naye hata hajaongelea mada za kukasirika basi kisaikolojia, mtu huyo huwa anajilinda asije akashutumiwa, kiufupi mtu huyo amekasirika kweli na hakuwa tayari kukubali). Kama mke wangu hakunishutumu kuwa mie, “wewe ni Muislamu”, sasa kwanini nijishtukie na kumwambia yale. Nililigundua hili, lakini bado nilisita. Kile kitambulisho kilichogandana namimi kwa miaka 43 bado hakikuwa rahisi kukiepuka.”

Lakini ilipofika Machi 1993, alishindwa kutoingia Uislamu. Mkewe pia wa miaka 33 akawa Muislamu pamoja naye. Baadhi ya sababu zilizosababisha kusilimu kwake zinaweza kufupishwa kama ifuatavyo:

** Hii ilikuwa ni Dondoo (excerpt) ya kitabu cha Salim Boss kiitwacho“Wao Ima ni Waerevu Mno au Wajinga Mno” chenye kurasa 672 zote zimechapishwa kwa rangi (full colour). Ni tarjama ya kitabu kilichouzika sana kiitwacho “They are Either Extremely Smart or Extremely Ignorant”  Kwa usomaji wa ziada tembelea www.extremelysmart.org au www.facebook.com/muerevumno “**

Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.