AR-RAHEEQ AL-MAKHTUM
Amri ya Kwanza ya Kudhihirisha Da’wa Jambo la mwanzo ambalo lilishuka kuhusiana na suala hili ni kauli yake Mwenyezi Mungu ﷻ Aliye Mtukufu:
وَأَنذِرْ عَشِيرَتَكَ الْأَقْرَبِينَ} الشعراء:214}
[Na uwaonye jamaa zako walio karibu nawe.] [26:214].
Hii ni aya kutoka katika Suratu Sshuaraa, ambamo ndani yake kimetajwa kisa cha Mussa (a.s.) tokea mwanzo wa Utume wake mpaka kuhama kwake pamoja na wana wa Israili, na kusalimika kwao kutoka katika makucha ya Firauni na watu wake, na kugharikishwa Firauni na watu wake. Kisa hiki kimekusanya hatua zote alizozipitia Musa (a.s.) wakati wa kumlingania Firauni na watu wake kumwelekea Mwenyezi Mungu ﷻ .
Ninaona kuwa kisa cha Nabii Musa kilielezwa wakati Mjumbe wa Mwenyezi Mungu ﷺ Alipoamrishwa kuwalingania . watu wake kumuelekea Mwenyezi Mungu ﷻ, ili uwe mbele yake na masahaba wake mfano wa yale ambayo watakutana nayo, katika mambo ya kukadhibishwa na kukandamizwa wakati watakapoudhihirisha ulingano, na imani yao tokea mwanzo wa Da’wa yao.
Kwa upande mwingine sura hii imekusanya pia maelezo ya kutajwa kwa mwisho mbaya wa watu wanaowakadhibisha Mitume, watu wa Nuhu, Aad, baadhi ya Thamud, watu wa
Ibrahim, watu wa Lut na Ashabul-Aykah (watu wa Mtume Shuaib); zaidi ya yale ambayo yametajwa katika mambo ya Firauni na watu wake. Kusudio ilikuwa ni kuwajuza wale ambao wangesimama na kukadhibisha ukweli walioletewa kuwa watapata adhabu kali kutoka kwa Mwenyezi Mungu ﷻ iwapo wataendelea na kukanusha ukweli ulio wazi mbele yao. Waumini wajue ya kuwa mwisho mwema ni wao na wala si wa wale wanaokadhibisha.