0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

KUHIMIZA KUFANYA KAZI YA HALALI

KUHIMIZA KUFANYA KAZI YA HALALI NA KUJIEPUSHA NA HARAMU

Nani katika sisi ambaye hataki kuwa na afya njema yeye na familia yake?. Yote hayo yanapatikana katika kuchuma halali.

Ndugu Muislamu, ukitaka afya njema na maisha mazuri hapa duniani na kesho akhera, jitahidi kutafuta riziki ya halali, ndio ufunguo wa kila kheri. Hakika Mwenyezi Mungu Ametuhalalishia vitu vingi vizuri, na Akatuharimishia vitu vichache viovu. Kila kitu ambacho kina manufaa kwa mwanadamu Allah kahalalisha na kila kitu ambacho kina madhara kwa mwanadamu, Allah kaharimisha. Ndugu Waislamu, hiyo ndio rehema ya Allah kwa waja wake baada ya kutuongoza katika Uislamu kisha aliwafundisha kila kitu ambacho mwanadamu anahitaji katika maisha yake, na akawatahadharisha na kila kitu ambacho kinadhuru maisha ya mwanadamu.

FADHILA ZA KUCHUMA MALI YA HALALI

Dini ya Kiislamu imeamrisha kuchuma halali na kuishi maisha mazuri. Imeamrisha watu kufanya kazi ya halali kwa bidii, kwa lengo la kujisaidia katika maisha. Na imekataza watu kuwa wavivu na kuomba omba njiani. Qur’an na Hadithi zimeweka wazi umuhimu wa kutafuta riziki na fadhila za kuchuma halali. Miongoni mwa fadhila za kuchuma halali:
Kuchuma halali na kula chakula cha halali ni njia ya Mitume. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

يَا أَيُّهَا الرُّسُلُ كُلُوا مِنَ الطَّيِّبَاتِ وَاعْمَلُوا صَالِحًا ۖ إِنِّي بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ}   المؤمنون:51}

[Enyi Mitume Kuleni vyakula vizuri na fanyeni mema. Hakika mimi ni Mjuzi wa yote mnayoyatenda].    [Al Muuminuun 51]

Na amesema Mtume ﷺ: [Hajakula mtu chakula kizuri kuliko chakula alicho kichuma kwa mikono yake, na Mtume Dawud alikuwa akila chakula kilicho chumwa na mikono yake]
Kutafuta chakula cha halali imeshikamanishwa na kwenda jihadi. Amesema Allah (Subhaanahu wa Taala):

وَآخَرُونَ يَضْرِبُونَ فِي الْأَرْضِ يَبْتَغُونَ مِن فَضْلِ اللَّهِ ۙ وَآخَرُونَ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللَّهِ}   المزمل:20}

[Na wengine watasafiri katka ardhi wakitafuta fadhila za Mwenyezi Mungu, na wengine watapigana katika njia ya Mwenyezi Mungu].    [Al Muzammil:20]
Kuamrishwa kutafuta riziki ya halali baada ya kutekeleza ibada tukufu ya Swala. Amesema Allah (Subhaanahu wa Taala):

فَإِذَا قُضِيَتِ الصَّلَاةُ فَانتَشِرُوا فِي الْأَرْضِ وَابْتَغُوا مِن فَضْلِ اللَّهِ وَاذْكُرُوا اللَّهَ كَثِيرًا لَّعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ}    الجمعة:10}

[Na itakapokwisha Sala, tawanyikeni katika ardhi mtafute fadhila za Mwenyezi Mungu] [Al-Jumaa:10]

Kuchuma halali na kula chakula cha halali ni sababu ya Allah (Subhaanahu wa Taala) kukubali dua zetu. Amesema Mtume ﷺ :

إن الله تعالى طيب لا يقبل إلا طيبا وإن الله أمر المؤمنين بما أمر به المرسلين فقال تعالى: { يَا أَيُّهَا الرُّسُلُ كُلُوا مِنَ الطَّيِّبَاتِ وَاعْمَلُوا صَالِحًا إِنِّي بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ}. وقال تعالى: { يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا كُلُوا مِنْ طَيِّبَاتِ مَا رَزَقْنَاكُمْ}. ثم ذكر الرجل يطيل السفر أشعث أغبر يمد يديه إلى السماء يا رب يارب ومطعمه حرام ومشربه حرام وملبسه حرام وغذي بالحرام فأنى يستجاب له رواه مسلم

[Enyi watu, hakika Mwenyezi Mungu ni mzuri, na hakubali ila kitu kizuri. Kisha akataja mfano wa mtu anaye safiri safari ndefu hali akiwa amechoka, nywele zake zimejaa vumbi, anainuwa mikono yake kuelekeza mbinguni huku akisema: Ewe Mola wangu, Ewe Mola wangu, na hali kwamba chakula chake ni cha haramu, Kinywaji chake cha haramu na mavazi yake ni ya haramu. Vipi Allah ataikubali Dua yake ].  [Imepokewa na Muslim]

ATHARI YA KUCHUMA CHAKULA CHA HARAMU

Hakika kuchuma haramu na chakula cha haramu kina athari mbaya kwa mwenye kuchuma na kadhalika kwa jamii nzima. Miongoni mwa athari hizo ni:
1. Kukosekana baraka na kuzidi ukame katika ardhi
2. Kuzidi magonjwa
3. Kuenea machafu katika ardhi
4. Dhulma na udhalimu kuzidi katika ardhi. Mfano wa watu kula mali kwa njia ya dhulma kama; kula Riba, kunyang’anya, kudanganya, kula Rushwa, na n.k.
5. Kupungua nafasi za kazi na kuzidi uhaba wa kazi
6. Dua kutokubaliwa
Ndugu Waislamu, mtu hawezi kuendelea katika maisha yake akiwa anachuma haramu. Vilivile, jamii haiwezi kuendelea ikiwa watu wake wanakula haramu. Leo watu hawachagui baina ya halali na haramu. Mtu hajali kula haramu na kulisha watu wake haramu. Amesema Mtume ﷺ:

يأتي على الناس زمان لا يبالي المرء ما أخذ منه، أمن الحلال أم الحرام]   رواه البخاري]

[Itawafikia watu wakati, mtu hatojali Aliyochukuwa ni katika halali au haramu]  [Imepokewa na Bukhari].

Ndugu Muislamu tujihadharini sana na kula haramu. Na tujuwe wazi ya kuwa Allah(Subhaanahu wa Taala)Atatuliza siku ya akhera kila tulicho kichuma hapa duniani. Je ulichuma kwa njia gani? Njia ya halali au ya haramu?. Tuandae jibu la kumjibu mola wetu siku hiyo nzito.

MIFANO YA WATU WEMA KATIKA KUJIEPUSHA NA HARAMU

Swahaba Abubakar Siddiq radhi za Allah ziwe juu yake aliletewa kitu na mfanyakazi wake. Abubakar akala, baada ya kula, yule mfanya kazi akamuliza Abubakar: Je wajua nimekipata wapi? Akasema Abubakar sijui. Akamuambia hicho kitu nilimdaganya mtu siku za jahalia(zama za ujinga)nilimfanyia uganga. Kisha akanipa hicho kitu ulicho kula kama zawadi. Abubakar akaingiza mkono wake mdomoni na akajitapisha na akatapika vyote vilivyokuwa tumboni.
Swahaba ‘Umar Bin Khattab radhi za Allah ziwe juu yake alikunywa maziwa, kisha akamuuliza yule aliyemletea maziwa: Je umepata wapi maziwa haya? Akamuambia nimechukuwa maziwa hayo kutoka kwa ngamia wa Sadaka katika Baitul maal. ‘Umar akaingiza mkono wake mdomoni na akajichapisha maziwa aliyokunywa.
Mmoja katika wanawake wema alimuusia mumewe kwa kumuambia: Ewe mume wangu mche Mwenyezi Mungu, hakika sisi tunaweza kuvumilia njaa, lakini hatuwezi kuvumilia ukali wa moto wa jahannam.
Ndugu Muislamu, hivi ndivyo walivyo kuwa watu wema wakishi, na ndio siri kubwa ya kufaulu kwao nayo ni kwa ajili ya kujiepusha na haramu. Kwa hivyo, ni jukumu letu sisi Waislamu kujiepusha na haramu na kujifananisha na watu wema. Kufanya hivyo ndio kufaulu kukubwa hapa ulimwenguni na kesho akhera.

SIKILIZA MADA HII NA SHEIKH YUSUF ABDI

Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.