MALCOLM X
Malcolm X alizaliwa kama Malcolm Little Mei 19, 1925 huko Omaha, Nebraska. Baba yake, Earl Little alikuwa mchungaji asiyeogopa kusema ukweli, na pia alikuwa msaada mkubwa sana wa kiongozi wa Harakati za Weusi (Black Nationalist) wakati huo, Marcus Garvey. Malcolm X alilelewa katika imani ya kisabato na mama yake.
Maisha ya Malcolm mwanzoni yalikumbwa na masaibu mengi. Kwa mfano, mwaka 1929 nyumba yao iliyopo Lansing, Michigan ilichomwa moto na kundi la wazungu lenye chuki; alikuwa na umri wa miaka sita tu wakati baba yake alipokufa katika kifo kibaya sana; mama yake akawekwa katika hospitali ya watu wenye matatizo ya akili (mtindio wa ubongo); akachukuliwa kwenda kulelewa katika vituo vya kulelea watoto wasio na uwezo; mwalimu wake alivunja ndoto zake za kuwa mwanasheria, alimwambia kazi hiyo haiendani na maniga (weusi), akamuusia awe fundi seremala akimsisitiza hata Yesu alikuwa seremala. Akaacha shule japokuwa alionesha ana uwezo mkubwa wa akili; akatumia sasa muda wake mwingi Boston, Massachusetts kufanya kazi za ajabu ajabu; japokuwa kazi yake ya mwanzo ilikuwa kung’arisha viatu; akasafiri kuhamia Harlem, New York ambapo akafanya uhalifu sana; kabla ya mwaka 1942, alikuwa mwongozaji vikundi vya madawa ya kulevya, umalaya, ukahaba, na kamari; na ilipofika mwaka 1946, alihukumiwa kwenda jela kwa miaka 10 kutokana na kukutwa na kosa la ujambazi (wizi wa kuvunja nyumba).
Malcolm X alijiongezea elimu yake wakati yuko jela. Ilikuwa humo humo gerezani ndio ambapo aliimeza Dictionary (aliihifadhi kichwani kamusi ya kiengereza yote), alisoma Biblia na kila kitu kuanzia somo linalohusu mabaki ya kale (Archeology) mpaka Somo la Uzazi na Kurithiana (Genetics). Wakati yupo humo gerezani, Malcolm akafata imani ya muislam mweusi na baada ya kuachiwa kutoka gerezani, akawa mjumbe katika Chama cha Waislamu Weusi (Nation of Islam) na kuchaguliwa kuwa msemaji wao. Nation of Islam ni kundi lilopotoka linalojinasibisha na Uislamu. Alijitoa toka katika Nation of Islam mwaka 1964 na kuanzisha kengine kiitwacho Muslim Mosque, Inc na pia akaunda Chama cha Umoja wa Wamerika Weusi (Organization of Afro-American Unity), kundi ambalo linatetea uzalendo wa watu weusi. Baadhi ya Waislamu wa Kisunni walimuusia sana Malcolm kuusoma Uislam wa kweli. Malcolm X alikubali ushauri ule ambao ukamfanya ajiengue kutoka katika Nation of Islam na baadae kukiri:
“Katika chuo kimoja na kengine ambapo nilipita kuongea katika mikutano isiyo rasmi, wengi kati ya watu weupe wamekuwa wakinifata wakijitambulisha kama waarabu, waMashariki-ya-Kati, au wanatoka kaskazini mwa Afrika na wapo hapa kimasomo, kikazi au wengine wana makazi ya kudumu. Wakawa wananiambia pamoja na maneno yangu ya kuwachukia wazungu, ni kweli sikosei ninavyojichukulia kuwa ni Muislamu lakini walihisi niusome vizuri Uislamu, nitauelewa na kuukubali. Kama mfuasi wa Elijah (kiongozi wa Nation of Islam), nilikasirishwa na walichokuwa wakinisema. Lakini baada ya hali hii kujirudia kwa muda, nikajiuliza mwenyewe, kama kweli mtu yuko kidhati katika kuitangaza na kuifata dini hii, iweje mtu arudi nyuma katika kujiongezea maarifa ya kuijua dini hiyo zaidi na zaidi?!…”
Mmoja wa hao Waislamu waliojitolea alikuwa Dkt. Mahmoud Youssef Shawarbi ambae nae aliongozwa na kauli ya Mtume “Mmoja wenu hawezi kuamini mpaka ampendelee mwenzake kile akipendacho nafsini mwake.”[1] alimshauri Malcolm kuukubali uislam wa kweli. Baadae Malcolm alifunga safari kwenda kuhiji Makkah ambapo aliugundua uislam wa ukweli na akawa muislam wa Kisunni akatoa shahada upya (mwenyewe) na kubadili jina lake kuwa Al-Hajji Malik Al-Shabbazz. Malcolm alikuwa na furaha baada ya kukamilisha Hijja yake akisema amefurahi kuwa mweusi wa kwanza kwa wazaliwa wa Marekani kuhijji. Siku zake za kuhiji zilileta mabadiliko kuhusu msimamo wake wa kuchukia weupe. Akasema:
“Kulikuwa na makumi elfu mengi ya mahujaji kutoka sehemu mbalimbali duniani, walikuwa watu wa rangi zote, kuanzia wale wazungu wenye macho ya rangi ya samawi mpaka Waafrika Weusi. Lakini wote tulikuwa tukishiriki katika ibada kuonesha imani ya mshikamano na umoja ambayo katika maisha yangu ya Marekani sikuwahi kuota kuwa itawezekana…Amerika inapasa kuufahamu uislam, kwa sababu hii ndio dini iliyoondoa tatizo la ubaguzi wa rangi katika jamii wakati dini hii iliposhushwa. Katika kuzunguuka kwangu katika mataifa ya Waislamu nimekutana, nimeongea na hata kula pamoja na watu ambao Marekani walikuwa wakichukuliwa ni weupe (wazungu).- lakini kwa hawa ile tabia chafu ya kibaguzi ya uweupe imeondoshwa katika fikra zao kwa Uislamu wao. Sijawahi kuona kabla, upendo huu wa dhati ambao hawa wanautekeleza bila kuzingatia tofauti zao za rangi.”
Wakati akiwa Hijja, aliandika barua kwa wasaidizi wake wa chama chake kipya (Muslim Mosque) kule Harlem na kuwaomba wazisambaze kwenye vyombo vya habari. Aliandika:
“Sijawahi kushuhudia ukarimu mkubwa na roho ya udugu wa kweli kama niliouona ule wa rangi zote kule ardhi takatifu, nyumba ya Ibrahim, Muhammad na mitume wote waliopita. Kwa wiki nzima sikuwa mzungumzaji ila ni kushangazwa tu kwa yale mapenzi yalioneshwa kwangu na wale watu wenye rangi tofauti….najua mnaweza kushangazwa na maneno haya yanayotoka kinywani mwangu. Ukweli hijja hii, imenilazimisha kubadili fikra zangu ambazo zilikuwa zimejaa mwanzoni na sasa nimeamua kutumia upande mwengine wa shilingi kwa baadhi ya mambo niliyokuwa nayaamini. Hili halijakuwa gumu kwangu. Japokuwa nimekuwa nikiiamini imani yangu kidhati, siku zote nimekuwa mtu mwenye kujaribu kukumbana na ukweli, na kuukubali uhalisia wa maisha. Siku zote nimekuwa ni mwenye kukiwacha kichwa changu wazi ili kiweze kwenda mkono kwa mkono na utafutaji mzuri wa ukweli. Katika kipindi cha siku hizi kumi na moja zilizopita, nimekula chakula kutoka katika sinia moja, nimekunywa kwa kutumia bilauri moja, na nimelala katika sehemu moja –huku tukiabudu kuelekea kwa Mungu mmoja- pamoja na Waislamu wenzangu, ambao macho yao ni ya rangi ya kisamawati kuliko! Wenye nywele zenye umanjano kuliko! Na wenye ngozi yenye weupe pe! Ila kwa maneno na matendo ya Waislamu hawa weupe, nimejihisi kama niko pamoja na wenzangu (Waislamu weusi) kutoka Nigeria, Sudan na Ghana. Kwa kweli kila mtu alikuwa kaka wa kweli kwa mwenzake, kwani ile imani ya kuabudia Mungu mmoja imeondoa kule kujiona kutoka vichwani mwao, kutoka tabia zao na hata kutoka katika hulka zao. Nimeona kweli kama wazungu wa Marekani wangekubali kuabudia Mungu mmoja basi bila shaka wangekubali umoja wa binadamu pia kuepuka kuwadhuru wenzao kwa sababu ya tofauti rangi tu. Kwa ubaguzi huu unaoenea Marekani kama saratani isiyo na tiba, tulitegemea wale wazungu wanaojiita wana mioyo ya kristo basi wangelivalia njuga tatizo hili kwa kufanya harakati za kulitokomeza. Huu ndio ulitakiwa uwe muda mahsusi wa kuiokoa Marekani kutokana na janga hili kubwa – janga lililoimaliza Ujerumani baada ya kuwamaliza Wajerumani wenyewe. Waliponiuliza kuhusu lipi lililokuvutia katika Hijja nikajibu ni huu udugu wa kweli, watu aina tofauti, wenye rangi tafauti, tokea maeneo tofuati duniani wanakuja kukaa pamoja na kuwa kitu kimoja! Kwa kweli jambo hili limenionesha nguvu za Upekee (U-moja) wa Mungu. Wote tumekuwa tukila kimoja, tukilala sehemu moja, kila kitu tulikifanya kwa pamoja katika kumuelekea Mungu mmoja.”
Malcolm X akarudi kutoka Hijja akiwa mtu tofauti, akiwa yuko katika silika yake ya asili kama alivyo mtoto asiye na dhambi hata kidogo, kabla ya kubadilishwa na mazingira. Mtume wa uislam, Muhammad alisema, “Yule anayekuja kwenye nyumba ya Mungu (Kaa’ba) akiwa na niya ya kuhiji na asiwe mwenye kusema au kutenda ovu, basi atarudi akiwa kama mtoto aliyetoka kwa mama yake punde.”[2]. Kutokana na hivyo, kule kuchukia weupe kwa Malcolm-X kulisafishwa baada ya kujifunza Uislamu huu wa kweli. Na tarehe 27 Disemba 1964, Malcolm alisema, “Nadhani hii ndiyo sababu kwanini Uislamu unaenea siku hadi siku. Uislamu hauna ubaguzi wa rangi hata kidogo katika mafundisho yake. Hakuna mafundisho yanayokutaka umhukumu mtu kwa rangi yake. Hata uwe na rangi gani katika Uislamu, utabaki kuwa Muislamu na utabaki kuwa ndugu yetu.”
Malcolm alibahatika kutembelea maeneo tofauti tofauti ulimwenguni na kukutana na watu mbali mbali wenye haiba kubwa. Miongoni mwa nchi alizotembelea ilikuwa ni Saudia Arabia ambapo alikutana na Muhammad Faisal; mjukuu wa mfalme; Ghana ambapo alikutana na Kwame Nkurumah, Misri ambapo alikutana na Gamal Abdel Nasser; Aljeria na kukutana na Ahmed Ben Bella, kiongozi mkuu wa mapambano ya Aljeria dhidi ya wakoloni Wafaransa, na alikuwa waziri mkuu wa mwanzo wa Aljeria (1962-63) na akawa rais wa kwanza (1963-65). Pia, Malcolm alitembelea Nigeria ambapo akafanya muhadhara mkubwa chuo kikuu Ibadan. Nchi nyengine ni Ethiopia, Tanzania, Guinea, Sudan, Senegal, Ufaransa, Liberia na Morocco. 21 Sept 1960, Malcolm alikutana na Fidel Castro katika hoteli ya Theresa, Harlem. Tarehe 3 Disemba mwaka wa 1964, Malcolm alikuwa Uingereza akishiriki mdahalo, Oxford. Yeye akawa upande wa kutetea kichwa cha mdahalo kilichobeba ujumbe “Siasa Kali (isiyo na kadiri) Katika Kuutafuta Uhuru Sio Kosa, na Siasa Poa (mwendo wa kiasi) Katika Kutafuta Haki Siyo nzuri.” Kwa Kiengereza kichwa cha mdahalo ni “Extremism in the Defense of Liberty is No Vice; Moderation in the Pursuit of Justice is No Virtue” Na mdahalo huo ulirushwa na televisheni kwa taifa zima na BBC. Katika mdahalo, Malcolm X alijitamba kwa fakhari kabisa, “Uislamu ni dini yangu, namuamini Allah, na namuamini Muhammad.”
Akiwa anafanya muhadhara katika ukumbi wa Manhattan 21 Februari 1965, washika mitutu watatu walimsogelea Malcolm karibu na jukwaa na kummiminia risasi 15. Malcolm akiwa na miaka 39, alitangazwa ameshaaga dunia mara tu mwili wake ulipowasili katika hospitali ya kidini ya Columbia, New York. Akazikwa katika makaburi ya Ferncliff huko Hartsdale, New York. Ossie Davis (1917-2005),(1)
** Hii ilikuwa ni Dondoo (excerpt) ya kitabu cha Salim Boss kiitwacho“Wao Ima ni Waerevu Mno au Wajinga Mno” chenye kurasa 672 zote zimechapishwa kwa rangi (full colour). Ni tarjama ya kitabu kilichouzika sana kiitwacho “They are Either Extremely Smart or Extremely Ignorant” Kwa usomaji wa ziada tembelea www.extremelysmart.org au www.facebook.com/muerevumno “**