AR-RAHEEQ AL-MAKHTUM
Mnamo siku ya Jumatatu tarehe nane mwezi wa Rabiul Awwal, mwaka wa 14 wa Utume nao ni mwaka wa kwanza wa Hijra sawa na 3/9/ 622 C.E., Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (ﷺ) aliwasili Quba. (1)
Urwah bin Al-Zubair (Radhi za Allah ziwe juu yao) alisema, “Waislamu wa Madina walisikia kuhama kwa Mtume (ﷺ) kutoka Makka, wakawa wanatoka kila asubuhi kwenda katika ardhi yenye mawe meusi kumngojea mpaka linawarudisha joto la mchana majumbani kwao. Siku moja baada ya kungoja kwa muda mrefu walipoingia majumbani mwao, alipanda mtu mmoja Myahudi juu ya majabali kwa shughuli zake binafsi, akamwuona Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (ﷺ) na Masahaba wake (Radhi za Allah ziwe juu yao), wakiwa na mavazi meupe. Myahudi hakuweza kusubiri na akasema kwa sauti yake ya juu: ”Enyi Waarabu babu yenu ambaye mnayemngojea, huyo anakuja.” Waislamu walisimama na kwenda kuchukuwa silaha zao (2)
Ibn Qayyim amesema, ”Kikasika kishindo cha Takbir kwa Banu Amri bin Aufi, na wakatoa Takbira Waislamu wengine kwa sababu ya furaha ya kuwasili kwake. Wakatoka kwenda kumpokea, wakamwamkia maamkizi ya ‘ Utume, wakamzunguka pembezoni mwake, kwa utulivu na wakati huo wahyi unashuka,
فَإِنَّ اللَّهَ هُوَ مَوْلَاهُ وَجِبْرِيلُ وَصَالِحُ الْمُؤْمِنِينَ ۖ وَالْمَلَائِكَةُ بَعْدَ ذَٰلِكَ ظَهِيرٌ
[..Kwam’ Mwenyezi Mungu ni kipenzi chake, na Jibril na Waislamu wema wote; na zaidi ya hayo Malaika pia watasaidia ] [66:4]
Abubakar (Radhi za Allah ziwe juu yao) alisimama kwa ajili ya watu na wakati huo Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (ﷺ) alikuwa amekaa, ikawa kila Answari ambaye -alikuwa bado hajawahi kumwuona Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (ﷺ) alikuja na kumuamkia. (Na katika mapokezi mengine) Jua lilipompata Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (ﷺ), Abubakar (Radhi za Allah ziwe juu yao) akaja na akamfunika kwa shuka yake, wakati huo ndio watu wakamjua Mtume wa Mwenyezi Mungu (ﷺ). (3)
Waislamu wa Madina walitoka kwa wingi kwenda kumpokea. Katika historia ya Madina hakujawahi kutokea siku ya furaha iliyowahi kushuhudiwa kama siku hiyo: Kwa hakika Mayahudi waliuona ukweli wa utabiri wa Mtume (ﷺ) kutoka kwa Nabii Habakuki, ”Kwa hakika Mwenyezi Mungu amekuja kutoka Tayman, na Kudusi kutoka milima ya Parani. (4)
Mtume wa Mwenyezi Mungu (ﷺ) alipofika Quba alifikia kwa Kulthum bint Hadim na wengine wanasema kwa Sa’ad bin Khaitham, kauli ya kwanza ndiyo iliyo na nguvu zaidi.
Ali bin Abu Twalib (Radhi za Allah ziwe juu yao) alikaa Makka kwa muda wa siku tatu, mpaka alipomaliza majukumu aliyopewa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (ﷺ) ya kurudisha amana za watu zilizokuwa kwake. Baada ya hapo naye akahama akisafiri kwa miguu, akaungana nao wakiwa Quba, na akafikia kwa Kulthum bint Hadim. Mtume wa Mwenyezi Mungu (ﷺ) alikaa Quba kwa muda wa siku nne, Jumatatu, Jumanne, Jumatano na Al khamisi, (5) na kuasisi Msikiti wa Quba na akasali ndani yake. Huo ndio Msikiti wa kwanza uliojengwa kwa ajili ya kumcha Mwenyezi Mungu (ﷻ) baada ya Utume. Ilipofika siku ya tano-Ijumaa-aliondoka kwa amri ya Mwenyezi Mungu (ﷻ), Abubakar akiwa nyuma yake, wakati huo amekwishapeleka ujumbe kwa Banu Najjari, wajomba zake, nao wakamuitika wakaja wakiwa wamezivaa panga zao. Wakaelekea upande wa Madina. Ijmnaa ikamkuta kwa Banu Saalim bin Aufi, akasali nao katika Msikiti ambao ulikuwa jangwani, na walikuwa kiasi cha watu mia moja.