MUSA CERANTONIA
Alizaliwa na kukulia Melbourne, Australia. Anatoka katika familia ya watoto 6. Alisilimu 2002 mwezi wa Ramadhani akiwa na miaka 17. Amesomea Historia na Mawasiliano (History and Communication) chuoni na baadae akajiendeleza kwa kusomea Historia ya Kiislamu. Amekuwa Rais ( Mwenyekiti ) wa Jumuiya ya Waislam wa Chuo Kikuu cha Victoria, hukohuko Melbourne. Ni baba wa watoto wawili, Aisha na Swafiyah. Musa ana asili ya Italia kwa baba, na mama mwenye asili ya Ireland. Italia likiwa taifa kiongozi kwa kufuata ukatoliki, kama ilivyotarajiwa, hata Musa Cerantonio naye alilelewa Kikatoliki. Alikuwa akiamini bila shaka kuwa kama Ukristo ndiyo dini yenye wafuasi wengi, na ukatoliki ambao yeye yumo ndani ndiyo kundi kubwa la Ukristo, bila shaka hiyo ndiyo dini ya kweli.
Sasa vipi alisilimu? Kama alivyojibu katika mahojiano, “ilikuwa safari ndefu iliyonichukua miaka miwili ya kusoma na kufuatilia Uislamu.” Na sasa twende tupite njia alizopitia yeye. Musa alisoma shule ya Msingi ya kikatoliki na kuingia shule ya sekondari ya kijamaa. Rafiki zake ambao wengine walikuwa waislam, walikuwa watumizi wa madawa ya kulevya na mengineyo ya kihuni, ila yeye alijilinda. Shule ya sekondari aliyoenda ilikuwa imejengwa kwa itikadi ya Kijamaa na hata katika midahalo ya shule, Musa alikuwa ‘akiwaka’ dhidi ya itikadi hizo za Kijamaa. Musa alipinga vikali mawazo ya kina Karl Marx aliyesema “dini ni kasumba tu ya watu” au “Mungu amekufa” ya Friedrich Nietzche. Ili Cerantonio aitetee dini yake, ilimpasa aisome na punde akaanza kusoma Biblia, alishtushwa na aliyoyakuta. “Baadhi ya visa vya Biblia ni vya kiasherati, ni vya kiponografia (matusi yenye kutia ashiki),”alisema, na kama mfano, Musa alitoa kisa cha Lut aliyeleweshwa na watoto zake wa kike. Sijui nimalizie!? Dah! Wacha niseme tu! Watoto wale wakafanya mapenzi na baba yao kwa masiku mawili ili kulinda nasaba ya baba yao (Mwanzo 19:30 – 36). Alishangaa inakuwaje visa kama hivyo viitwe Neno la Mungu? Hii ndiyo sababu ya Dkt. Lawrence Brown, mchungaji, hakuamini ile kauli inayosema ati “Maandiko yote Matakatifu yameandikwa kwa uongozi wa Mungu, na yanafaa katika kufundisha ukweli, kuonya, kusahihisha makosa, na kuwaongoza watu waishi maisha adili” [2 Timotheo 3:16, Biblia-Habari Njema (Good News)] ya visa hivyo. Katika kitabu chake, MisGoded, Dkt. Brown aliandika kuwa, katika Biblia:
“….Kuna hadithi za walevi walio uchi, kujamiiana kwa maharimu (au ndugu) na umalaya ambao hamna mwenye haya anayeweza kumsomea mama yake, au kwa watoto wake. Na bado, moja ya tano ya kundi la watu duniani linakiamini kitabu kinachosema Nuhu “akanywa divai, akalewa; akawa uchi katika hema yake.”( Mwanzo 9:22 ) na kile cha,
“Lutu akapanda kutoka Soari akakaa mlimani, na binti zake wawili pamoja naye, kwa sababu aliogopa kukaa katika Soari. Akakaa katika pango, yeye na binti zake wawili. Yule mkubwa akamwambia mdogo, Baba yetu ni mzee, wala hakuna mtu mume katika nchi atuingilie kama ilivyo desturi ya dunia yote. Haya, na tumnyweshe baba yetu mvinyo, tukalale naye, ili tumhifadhie baba yetu uzao. Wakamnywesha baba yao mvinyo usiku ule, akaondoka huyo mkubwa akalala naye, wala yeye hana habari alipolala wala alipoondoka. Ikawa siku ya pili, mkubwa akamwambia mdogo, Tazama, nimelala jana na baba yangu, tumnyweshe mvinyo tena usiku huu, ukaingie ukalale naye. Wakamnywesha tena baba yao mvinyo usiku ule, akaondoka mdogo akalala naye, wala yeye hana habari alipolala wala alipoondoka. Basi hao binti wote wawili wa Lutu wakapata mimba kwa baba yao.” [Mwanzo 19:30-36]
Kwa maelezo kamili na ushahidi kuhusu hadithi zenye uasherati na kupotoka kama ukahaba na zinaa angalia (Mwanzo 38:15 – 26), kuhusu ukahaba (Kitabu cha Waamuzi 16:1), mkengeuko (2 Samweli 16:20 – 23), umalaya (Ezekiel 16:20 – 34 na 23:1 – 21), uzinzi (Methali 7:10 – 19), ubakaji baina ya ndugu kama ule aliofanyiwa Tamari katika 2 Samweli 13:7 – 14 inaonesha maadili ya ajabu, na Tamari (aliyebakwa) alishauriwa kwa kuambiwa, “sasa tulia, dada,” kwani, “[Huyo mbakaji, Absalomu] ni nduguyo; usilitie moyoni jambo hili.” (2 Samweli 13:20). Mh! Mbakaji akiwa kaka yako hakuna tatizo!!? Je ni kweli tuendelee kuamini “Hekima” hizi ni matendo ya uteremsho kutoka kwa Mungu?, au ndoto chafu tu?[1]
Mshituko mkubwa kwa Musa ulikuja pale alipogundua kuwa sheria za Biblia hazifuatwi na Wakristo. Mathalan, aligundua kutoka katika Biblia kuwa wanaume wanapaswa kufuga ndevu lakini Papa na Wakristo wengi wananyoa. Biblia inaelekeza watu waepuke mvinyo lakini kanisani Jumapili, mchungaji anawapa wanywe; Biblia inakataza kula nyama ya nguruwe lakini wengi wa Wakristo wanaifanya nyama ya mnyama mchafu huyo na mwenye magonjwa mengi kuwa chakula chao kipenzi. Musa akaamua kufuata amri za Biblia, akaanza kufuga ndevu na kuacha pombe na nguruwe. Familia ilipomuuliza akajibu, “Biblia ndivyo inasema.” Wakawa wanamuwakia kumwambia, “hilo ni Agano La Kale.” Na yeye akashangaa inakuwaje wakataze maneno ya Mungu na kufuata baadhi! Musa Cerantonio akaamua kuwapa changamoto kwa kuwauliza, “Mnakubali ndoa za Jinsia moja?.”
Bila shaka jibu ni “hapana” ndipo Musa akawambia kuwa kupigwa marufuku kwa ndoa hizo zatokana na Agano La Kale. Akaona huu ni unafiki kufuata baadhi ya sheria na kuacha nyengine.
Musa hakuwa na furaha kwa kitendo kile cha kuchagua ya kufuata na mengineyo ya kuyaacha, ndiyo sababu wakati mwingine alichukulia Ukristo kama mgahawa, ambapo unaenda unaagiza chakula ukitakacho na kwa vile usivyotaka vinakuwa havikuhusu.
Katika mahojiano yake na Saudi Gazette, aliombwa ahadithie alivyopita katika njia mpaka akaufikia Uislamu, Musa alijibu kwa kusema:
“ Nilikuwa nikisoma Biblia na nikagundua nguruwe ni haramu, lakini Wakristo cha kushangaza wanakula. Nikashangaa kuona Wakristo wasivyoifuata Biblia. Nikajiona nasogea karibu na uislam na hapo nikaamua kusoma. Niligundua kumbe hadi Waislamu wanamuamini Yesu (Amani iwe juu yake). Nikajiambia, inaonekana Uislamu ni mzuri ngoja niusome zaidi.”
Kwa hamu yake ya kuujua ukweli, Musa alitembelea Vatican mwaka 2000. Jiji la Vatican ni dola huru iliyo ndani ya jiji la Rome, Italia. Ulikuwa ni mwaka wa Jubilii (Sikukuu ya Ukumbusho) ambayo kwa ukatoliki ulikuwa ni mwaka maalumu wa kutolewa dhambi na kuomba msamaha. Aliambiwa, mtu akiingia kupitia “ mlango mtakatifu” (unaojulikana kama Porta Santa kwa lugha ya Italia), madhambi yake yote yanapukutika. Musa hakulimezea hilo bali aliuliza, “Jambo hili limezungumzwa wapi katika Biblia!?” na hakupata majibu ya kumridhisha. Na alipoamua kuingia kupitia mlango ule, alishituka kuona mwili uliokaushwa wa mapapa wa zamani na chakushangaza zaidi, watu walikuwa wakiuabudu. Aliona pia watu wakifuta miguu ya sanamu na kuomba waliyoyataka. Akaingia hadi chumba cha Papa (Capella Sistina) na akaona kwenye dari kuna michoro mbalimbali ikiwemo picha ya Mungu mwenyewe (alieonekana kama kikongwe na mwenye ndevu zenye mvi) na Adam! Hakuweza kushabihisha alichoona na amri ya pili ya Biblia: “Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.” [Kutoka 20:4]. Musa Cerantonio alipinga yote hayo na akaanza kujiita Mkristo asiye na dhehebu lolote, mtu fulani anaye amini Mwenyezi Mungu na asifate kanisa lolote. Na ilikuwa ni katika kipindi hiki ndipo alipoanza kusoma dini nyingine kama Uhindi, Ubudha, Shinto, lakini kamwe hakufikiria Uislam.
Baada ya kipindi fulani, alijitokeza Muislamu aliyemwambia, “Naona faraja kukutana na wewe, jina langu ni fulani, je ungependa kuwa muislam?” Hili lilifungua milango kwa yeye kujifunza uislam kwani kwa chochote Musa alichotaka kujua katika uislam alimuuliza mtu huyo. Muislam huyu alimpatia Musa Qur’ani, lakini Musa hakuisoma. Musa aliipokea tu Qur’ani na akaihifadhi pahala, kaka yake alipoigundua kuwa ni Qur’ani, aliichukua na kuichoma. Kuna wakati alikutana na marafiki zake Waislamu, miongoni mwa hao waislam, mmoja wao alikuwa haujui uislam vizuri. Katika maongezi yao na Musa, alikuwa akimtusi Yesu bila ya kujuwa kuwa alikuwa mmoja wa Mitume wakubwa wa Allah. Hili lilimjaza wahaka Cerantonio na akaamua kidhati kuusoma uislam ili kuishambulia imani hiyo ya waislam. Katika kusoma kwake, cha kwanza alichogundua kilikuwa ni waislam wanamuamini Yesu Kristo. Lingine aligundua kuwa Waislam wanaamini Mungu Mmoja na hawamshirikishi. Kila alivyousoma zaidi, ndivyo alivyotaka kuujua zaidi. Kwa vile alivyokuwa ameusoma Uislamu kiundani na kuuelewa, ilifika kipindi hadi baadhi ya rafiki zake Waislam walikuwa wakimfuata na kumuuliza maswali mbalimbali ya kiislamu (wakitaka wapewe Fatwah kuhusu hayo maswala yao). Kipindi muhimu kilicholeta athari kubwa ni pale rafiki yake mmoja alipompa DVD ya Abdul-Rahim Green (Mzungu aliesilimu vilevile), inaonesha jinsi alivyosilimu. Baada ya kuangalia video ile, Musa akajitangazia kuwa yeye si Mkristo tena, sio Mkristo na sio Muislam. Ila alianza kufuata matendo ya kiislam kama kuswali kwa kusujudu. Alikuwa bado hajasilimu, na mwezi wa Ramadhani ulipowasili, aliwauliza rafiki zake waislam kama watafunga, alishangazwa kusikia kuwa baadhi yao hawatafunga. Ila yeye alisema, “ Mimi siyo muislam, ila nitafunga mwezi mzima.” Na ukweli ukawa kama alivyo ahidi, kwani mwezi mtukufu ulipowasili, alifunga na kufuturu nyumbani kwa rafiki zake. Alichopendelea zaidi ni “misosi” (vyakula) vilivyopikwa na kupikika vya Waislamu. Hapo nyumbani kwa rafiki yake, alikiona kitabu kimoja kiitwacho “A Brief Illustrated Guide To Understanding Islam” (Mwongozo Mfupi Wa Kuuelewa Uislamu) kilicho haririwa na I.A Ibrahim kilichoongelea miujiza ya Qur’an Tukufu. Musa hakujizuia kukisoma kitabu kile. Na alipomaliza tu , alitamka shahada, “Ash-hadu anlaa ilaaha ila LLah, wa Ash-hadu anna Muhammadan Rasuulullah”, ikimaanisha kuwa, “ Nashuhudia (nakiri) hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah, na Muhammad ni Mtume Wake.”
Musa Cerantonio amesafiri sehemu nyingi za dunia. Na mwaka 2005, alitembelea mji mtukufu wa Madinah. Alikwenda kuishi Misri, na akafanya kazi katika chaneli ya televisheni ya kiislamu inayotumia lugha ya Kiingereza. Katika mahojiano fulani, Yosra Mmarekani aliyesilimu, alimuomba Musa, “………elezea jambo moja lililokuvutia hapa Misri hata ukadiriki kutosita kutamka neno ‘SubhaanAllah’ na Cerantonio alijibu,
“Nakumbuka siku niliyowasili nyumbani kwangu, nilimuuliza mlinzi wapi kuna msikiti uliokaribu na hapa. Aliniambia kuwa, kama nikienda kushoto ipo miwili, nikienda kulia upo mwingine, nikienda moja kwa moja, nitakutana na miwili, pembeni ya gorofa ninalokaa kuna masjid nyengine. Na yote ilikuwa haikuchukui zaidi ya dakika 1. Nimetoka sehemu yenye msikiti mmoja katika eneo zima, nimekuja sehemu nayochagua msikiti upi niswali katika minane iliyopo karibu!”
Mara ya kwanza kwenda kuhiji ni 2006, na mara ya pili ni 2011. “Sina maneno kuelezea hilo,” Musa alijibu kuhusu alivyojisikia alivyokuwa akihiji, “kwa ujumla ilikuwa faraja. Haikuwa kama nilivyotarajia. Nimejifunza kuhusu umoja wa umma wa Kiislam. Hija pia inakufundisha kuwa mvumilivu. Nimerudi nikiwa mtu mwengine hata familia yangu na marafiki waliligundua hilo.” Katika mahojiano yaliyochapishwa na The Saudi Gazette, Musa aliulizwa ushauri wake kwa vijana wa Kiislamu, ambapo alisema,
“ Unaona jinsi Magharibi inavyokuwa ya Waislamu; wanamuziki, matajiri na watu wengine mashuhuri wote wanaingia katika Uislamu. Vijana wa kiislamu inapaswa wajiulize inakuwaje watu hawa walioyashinda maisha wawe na pupa hivi kuingia katika Uislamu. Ni kwa sababu ni dini ya haki na wanataka pepo pia. Tambeni kwa kuwa Waislamu.”
Akiongozwa na shauku ya kutaka radhi na thawabu za Allah kwa kuwaita watu katika uislam, Musa Cerantonio amejumuika katika majukwaa tofauti kutangaza Uislamu. Ni mara mbili kashawahi kuhudhuria Kongamano kubwa la Amani la Kiislamu (Islamic Peace Conference) lililofanyika Mumbai mwaka 2007 na 2009, vile vile ameweza kuhudhuria Kongamano kama hilo la Dubai (Dubai Peace Conference) la mwaka 2010. Amefanya mihadhara kuhusu Uislamu katika hafla mbalimbali sehemu nyingi kama Australia, India, UAE, Ufilipino, Kuwait na Qatar. Amefanya kazi Iqraa International, chaneli ya televisheni irushwayo katika satelaiti.katika moja ya vipindi vyake vinavyorushwa na Iqraa International, Musa alimuhoji Lauren Booth, shemeji wa aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza, Tony Blair. Lauren Booth ambaye naye ni mtangazaji, aliingia katika dini hii ya Kiislamu katikati ya mwezi Septemba 2010 na alipania kwenda kuhiji mwaka 2011. Katika mahujiano hayo yaliyofanyika Madinah Al-Munawwarah, Cerantonio alitaka kujua jinsi alivyosilimu na aliuliza pia anavyojisikia akiwa na dini mpya. Kama unatatizwa na swali lolote ambalo unahitaji jibu lake, basi usisite kumuuliza Cerantonio kwani yuko tayari kulijibu papo kwa papo kupitia kipindi chake “Ask the Sheikh” (Muulize Sheikh) kinachorushwa na Iqraa International.
Musa pia ametokea katika chaneli ya muda wote ya bure, Peace TV. Katika moja ya kipindi chake, Musa alitoa “Ushari kwa Waislamu Kutoka kwa Waliosilimu” na anakiri baadhi ya waislamu ndio sababu ya kuzuia watu wasiingie katika Uislamu. Kwa mfano Musa anahadithia kuwa kabla hajasilimu, rafiki yake Muislamu alimsihi Musa asisilimu. Kisa na maana ni kuwa, endapo Musa atasilimu, wazazi wake watakereka na kukasirika, wakitaka kujua, “Nani aliyemsababisha mpaka mtoto wetu akasilimu, nani aliyemvuta katika Uislamu, nani aliyesababisha mwenetu atengane na familia yake na mila zake…” Musa akasema, Waislamu wanawazuia wasio Waislamu kuingia katika dini yao. Na hili linasababishwa na matendo yao. “Kumbuka tabia yako ndio Daawah yako” kwa hivyo Waislamu inabidi watumie tabia zao njema kutangaza dini. “Wengi wa Waislamu niliokutana nao,” Alikiri, “walikuwa na tabia mbaya, wanakuibia, wanaongopa, walikuwa wanafanya kila kitu ambacho Muislamu hatakiwi kukifanya.” Cerantonio aliwaonya watu wasiwe na tabia ya kulaumu gari katika ajali bali walaumu dereva . “Kwa bahati nikaelewa labda haya ni yale wanayofanya Waislamu lakini kuna lile ambalo Uislamu unalifundisha wacha nilisome hilo.” Musa anaona tabia ya mtu ni njia bora ya kuusambaza Uislamu hivyo anawausia Waislamu wajipambe na tabia hizo njema. Anasema unaweza kufanya jitihada ya kumgaia asiye Muislamu kitabu lakini asikisome, unaweza kumpa CD ya mawaaidha na bado asiisikilize, pia unaweza mkabidhi DVD ya kiislamu na bado asiangalie, sasa ufanyeje ukifikiwa na ugumu huu? Basi jitahidi uwezavyo kutoa Daa’wah kupitia tabia zako. Ushauri huu wa Cerantonio unawafikiana na ule wa mwanazuoni wa kiislamu aliyewaambia wanafunzi wake, “Waiteni watu katika Uislamu huku mkiwa kimya.” Wanafunzi walishtuka, wasijue ni kwa vipi wanaweza waita watu katika Uislamu bila kunyanyua ndimi zao, naye akawajibu, “Kwa kutumia tabia zenu.”
Cerantonio anaelekeza kuwa, jirani yako, rafiki yako ni Muislamu mtarajiwa kwa hivyo usidharau juhudi zao za kuwabadili watu. Yeye mwenyewe alivutika na Uislamu pia kwa kujua Yesu anameremeta kwa Waislamu. Alishasema, ikiwa utamueleza anayejiita mfuasi wa Kristo kuwa sisi waislmu tunampenda Yesu kuliko yeye basi anaweza kuvutika kujifunza Uislamu. Katika kipindi kimoja cha Peace TV: “My Choice”, Musa alifunga kipindi hicho kwa dua ifuatayo: “Namuomba Allah atufanye tuwe waumini wa kweli wa Tauhiid (kumfanya Mola kuwa mmoja kikweli kweli), tuwe miongoni mwa wale wasiomshirikisha na lolote, na tusimsifu yeye Mungu kwa sifa ambayo hajajisifu nayo Yeye Mwenyewe.” *
** Hii ilikuwa ni Dondoo (excerpt) ya kitabu cha Salim Boss kiitwacho“Wao Ima ni Waerevu Mno au Wajinga Mno” chenye kurasa 672 zote zimechapishwa kwa rangi (full colour). Ni tarjama ya kitabu kilichouzika sana kiitwacho “They are Either Extremely Smart or Extremely Ignorant” Kwa usomaji wa ziada tembelea www.extremelysmart.org au www.facebook.com/muerevumno “**