KUTAHADHARI NA UZUSHI KATIKA DINI
Shukrani za dhati ni za Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala Aliyesema:
{الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا} المائدة :3
[Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini. ] [Al-Maaida:3]
Na rehma na amani zimfikie Mtume wetu aliyesema:
[من أحدث في أمرنا هذا ما ليس منه فهو رد ] رواه البخاري ومسلم
[Atakayezusha katika jambo letu hili (Dini) ambalo si katika dini atarudishiwa mwenyewe]. [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
Tumcheni Mwenyezi Mungu Ambaye amemtumiliza Mtume Muhammad pale walipokuwa watu wako katika upotofu wa ushirikina na kufuata dini ya baba zao potofu. Akawatoa katika ushirikina na kuwaleta katika Uislamu (Dini ya haki). Kwa Kweli, Mtume ﷺ alisubiri mengi maovu aliyotendewa na waovu mpaka Dini ikakamilika.Pia aliweza kuwatahadharisha watu na kufuata hawaa zao na kuzusha katika Dini ya Mwenyezi Mungu baada ya kuondoka yeye.
Kwa kweli uzushi katika dini ulianza punde tu baada ya kuondoka Mtume ﷺ, kwani vipote vingi vilizuka kwa sababu ya watu kuacha Sunna ya Bwana Mtume ﷺ na kufanya mambo bila ya elimu na kufuata matamanio ya nafsi. Na mfano wa vikundi hivyo ni Muutazila, Masufi, Khawaarij, Murjia na vikundi vyengine. Kuna ushahidi mwingi wa kushikamana na sunna na kujiepusha na bidaa. Mola Subhaanahu wa Taala Amesema:
{قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَاللَّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ} آل عمران: 31
[Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu.] [Al-Imraan:31]
Pia Mwenyezi Mungu amesema:
{وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ وَاتَّقُوا اللَّهَ ۖ إِنَّ اللَّهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ} الحشر:7
[Atakachowapeni Mtume kichukueni na atakachowakataza jiepusheni nacho] [Al-Hashri:7]
Mtume ﷺ amesema:
[من أحدث في أمرنا هذا ما ليس منه فهو رد ] رواه البخاري ومسلم
[Atakayezusha katika Dini yetu hii jambo ambalo halimo katika Dini basi atarudishiwa mwenyewe]. [Imepokewa na Bukhari na Muslim ]
Vile vile Mtume ﷺ Asema katika hadithi yake:
[فمن رغب عن سنتي فليس مني] رواه البخاري ومسلم
[Anayejiepusha na sunna yangu si katika mimi]. [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
Na katika hadithi nyingine Mtume anasema:
أخرج ابن ماجه عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَبَّاسٍ، قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: أَبَى اللَّهُ أَنْ يَقْبَلَ عَمَلَ صَاحِبِ بِدْعَةٍ حَتَّى يَدَعَ بِدْعَته. ضعفه الألباني
Amepokea Ibnu Maajah kutoka kwa Ibnu Abbas radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake amesema : Amesema Mtume rehma na Amani zimfikie yeye [Anakataa Mwenyezi Mungu kukubali amali ya mtu mzushi mpaka ache uzushi]. Lakini sheikh Al-Albaniy ameidhofisha Hadithi hii
Na amesema Mtume rehma na amani zimfikie yeye:
[وإياكم ومحدثات الأمور، فإن كل محدثة بدعة وإن كل بدعة ضلالة] رواه أبوداود
[Jiepusheni na kuzusha mambo (katika dini) kwani kila uzushi ni upotofu]. [Imepokewa na Abuu Daud]
Inatakiwa waumini washikamane na Sunna na wajiepusha na uzushi katika Dini. Kwani ndiko kumkubali kikamilifu Bwana Mtume ﷺ, na pia kumtii yeye. Wala haifai kwa Muislamu kwenda kinyume na Sunna ya Mtume ﷺ. Ametahadharisha Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) hilo aliposema:
{فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ} النور:63
[Na wajitadhari wanaokhalifu amri ya Mtume wasije wakapata fitna au adhabu kali ] [Al-Nnuur:63]
Vilevile, Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala Anasema:
{وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ ۗ وَمَن يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا} الأحزاب:36
[Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapo kata shauri katika jambo lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi.] [Al-Ahzaab: 36]
Aya hizi zanaonesha kwamba yoyote atakayemuasi Mola na Mtume atakuwa katika upotevu na kupata adhabu kali ya Mwenyezi Mungu
Ndugu Muislamu kwenda kinyume na Sunna ya Mtume ﷺ ni sababu ya kufarakana Waislamu katika Dini na kupotoka upotevu ulio wazi, Amesema Mola Subhaanahu wa Taala:
{وَهَٰذَا صِرَاطُ رَبِّكَ مُسْتَقِيمًا ۗ قَدْ فَصَّلْنَا الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَذَّكَّرُونَ} الأنعام:126
[Na hii ndiyo Njia ya Mola wako Mlezi Iliyo nyooka. Tumezipambanua Aya kwa watu wanao kumbuka.] [Al-An’aam:126]
Vilevile, kukhalifu Sunna ni sababu ya mtu kufuata matamanio ya nafsi. Na Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala Ametutahadharisha kufuata matamanio kwa kusema:
{أَفَرَأَيْتَ مَنِ اتَّخَذَ إِلَٰهَهُ هَوَاهُ } الجاثية:23
[Je! Umemwona aliye fanya matamanio yake kuwa ndiye mungu wake,] [Al-Jaathiyah:23]
Na wanaofuata matamanio ni wale ambao Mwenyezi Mungu(Subhaanahu wa Taala) Aliwataja kwa kusema:
{أُولَٰئِكَ الَّذِينَ طَبَعَ اللَّهُ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ وَاتَّبَعُوا أَهْوَاءَهُمْ} محمد:16
[Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao, na wakafuata pumbao lao.] [Muhammad:16]
Uzushi katika Dini, Mtume ameuita kuwa ni upotofu kwa sababu mzushi amepotea kwa kufuata matamanio. Tusisahau Mtume ﷺ alikuwa akijilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na tabia mbaya, na kufuata matamanio ya moyo. Enyi waja wa Mwenyezi Mungu ! Haifai kwa mtu yeyote kuleta maoni yaliyo kinyume na Sunna ya Bwana Mtume ﷺ. Amesema ‘Abdillahi Ibn ‘Abbas: (R.A.) “ Atakayeleta maoni ambayo hayapo katika kitabu cha Mwenyezi Mungu wala hadithi za Mtume ﷺ kwani hajui yatakayompata yeye atakapo kutana na Mwenyezi Mungu ﷺ
Jueni kuwa mzushi ni dhalili na pia ana hasira za Mwenyezi Mungu aliyetukuka. Amesema Imam Shatwiby, Mwenyezi Mungu amrehemu: “Hakika mzushi atavishwa udhalili duniani na hasira za Mwenyezi Mungu”. Na hii ni kwa neno la Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala Aliposema:
{إِنَّ الَّذِينَ اتَّخَذُوا الْعِجْلَ سَيَنَالُهُمْ غَضَبٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَذِلَّةٌ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۚ وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُفْتَرِينَ} الأعراف:152
[Hakika wale walio muabudu ndama, itawapata ghadhabu ya Mola wao Mlezi na madhila katika maisha ya dunia. Na hivi ndivyo tunavyo walipa wazushi.] [Al-A’raaf:152]
Adhabu hii itakuwa pia kwa wale wanaofanana nao kitabia kwani uzushi ni kumsingizia Mwenyezi Mungu. Asema Imam Malik Mwenyezi Mungu amrehemu:
من ابتدع في الاسلام بدعه يراها حسنه فقد زعم ان محمدا ( صلى الله عليه وسلم ) خان الرسالة لان الله يقول ( اليوم أكملت لكم دينكم ) فما لم يكن يومئذ دينا فلا يكون اليوم دينا
“Atakayezusha katika Uislamu uzushi, akauona uzushi huo ni mzuri basi amedai ya kwamba Mtume Muhammad ﷺ amefanya khiana katika ujumbe, kwani Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala Amesema: “ Leo nimewakamilishia Dini yenu”. Kwa hivyo, lile ambalo halikuwa siku hiyo Dini basi leo haliwi dini’.
Na ameweka bayana Mtume kama ilivyo katika sahihi Muslim kwamba wazushi watasogea katika birika la Mtume ﷺ na watafukuzwa kwa sababu ya uzushi wao unamaliza Dini sahihi ya Mwenyezi Mungu.
SIKILIZA MADA HII NA SHEIKH ALI BAHERO