ATAFANYA NINI MTU ANAESWALI SWALA YA SUNNA KISHA IKAKIMIWA SWALA?
Suali:
Ikiwa naswali kisha swala ikakimiwa, jee nitoe salamu na nijiunge na Swala ya Jamaa ama nikamilishe Swala ya Sunna ?
Jawabu :
Amepokea Imamu Muslim (710) kutoka kwa Abii Hureira radhi za ALLAH ziwe juu yake kutoka kwa Mtume MUHAMMAD ﷺ anasema :
[إذا أقيمت الصلاة فلا صلاة إلا المكتوبة]
[Inapokimiwa Swala basi hakuna Swala nyengine isipokua Swala yafaradhi].
Hadithi hii inaonesha yakwamba inapokimiwa Swala haifai kwa yeyote kuanza kuswali Naafilah yaani swala ya sunna.
Anasema Ibnu Qudamah ALLAH amrehemu “Na Swala inapokimiwa ,hatoshughulika mtu na swala hiyo kwa kuswali Naafilah yaani sunna , sawa atahofia kupitwa na rakaa ya kwanza ama hatohofia. na hii ndio rai aliyoisema Abu Hureira, na Ibnu Umar, na Urwah , na Ibnu Syriin , na Saeed bin Jubair , na Shafi’i , na Ishaq , na Abu Thaur”
Kutoka katika kitabu cha [Al Mughni] (1/272)
Na wakatolea dalili hadithi hii tena baadhi ya Wanazuoni yakwamba yule anaeswali Sunna kisha Swala ya faradhi ikakimiwa basi ataikata ile sunna.
Anasema Al Haafidh Al Iraqiy : “neno yake Mtume ﷺ : “[Hakuna swala] Kuna uwezekano inakusudia: asianze mda ule kuswali swala inapokimiwa , na pia kuna uwezekano inakusudia :Asijushughulishe na Swala hata kama amaeianza kabla ya kukimiwa Swala bali ataikata Swala ile mwenye kuswali ili aipate fadhla ya Takbira ya kwanza , au swala ile ya sunna inabatwilika yenyewe hata kama hatoikata mwenye kuswali , kuna uwezekano wa mambo haya yote mawili”
Na pia imenukuliwa kutoka kwa Sheikh Abii Haamid kutoka katika Madhehebu ya Imam Shafi’i yakwamba ni bora kwa mtu kuacha kuswali Sunna ikiwa kukamilisha kwake Sunna ile kutamfanya akose fadhla ya Takbira ya ihram yaani Takbira ya kufungua Swala. [Maneno ya Al Iraqy ameyanukuu Shaukany katika [Nailul awtwaar 3/91].
Na fatwa hii ndio iliyotolewa na kamati ya kudumu ya Fatwa nchini (Saudi arabia) pale ilipoulizwa kamati hiyo : Jee inafaa nikate kuswali Naafilah (sunna) na nikimbilie Takbira ya Ihram pamoja na imam ama nikamilishe Naafilah Swala ya Sunna ??
Kamati ya fatwa ikajibu :
“Ndio swala ya faradhi inapokimiwa basi kata sunna ambayo upo ndani yake ili upate Takbira ya ihram pamoja na imam kwa yaliyothibiti katika maneno ya Bwana Mtume ﷺ:
إذا أقيمت الصلاة فلا صلاة إلا المكتوبة
[Swala inapokimiwa basi hakuna Swala nyengine isipokua Swala ya faradhi]
[Fatwa za kamati ya kudumu (7/312).]
Na amerajihisha Sheikh ibnu Uthaymeen Mungu amrehemu yakwamba inapokimiwa Swala na mtu yupo katika Rakaa ya kwanza katika Swala ya Sunna basi ataikata Sunna ile, na ikikimiwa na yeye yupo katika Rakaa ya pili basi ataikamilisha haraka haraka kwa uwepesi walo hatoikata.
Anasemaa Sheikh Ibnu Uthaymeen ALLAH amrehemu.
Na tunayoyaona katika Mas’ala haya :ni yakwamba ukiwa katika rakaa ya pili basi kamilisha kwa uwepesi, na ukiwa katika Rakaa ya kwanza basi ikate hiyo sunna . na maegemeo yetu katika hayo ni maneno ya Mtume ﷺ aliposema :
[من أدرك ركعة من الصلاة فقد أدرك الصلاة] رواه البخاري (580) ومسلم (607
[Atakaediriki na kupata Rakaa moja katika Swala basi amaediriki Swala nzima]
[Imepokewa na Bukhary (580) na muslim (607).]
Na huyu alieswali Rakaa moja kabla ya kukimiwa Swala anakua amepata Rakaa katika Swala iliyosalimika na pingamizi nalo ni kukimiwa swala, kwahivyo anakua amepata swala kwa kupata kwake rakaa kabla ya makatazo basi na aikamilishe kwa uepesi ……. Kisha akasema : na hili ndilo ambalo zimekusanyika kwake dalili zote” [Al sharhul mumti’i” (4/238).]
Na mtu anapokata Swala ya Sunna basi anaikata bila ya salamu.
Iliulizwa kamati ya kudumu ya Fatwa nchini (Saudi arabia) (7/312)
Ikikimiwa swala na ikawa kuna mtu anatekeleza Rakaa mbili za Sunna au Tahiyyatul masjid jee atakata swala yake ili aswali faradhi pamoja na jamaa ?. Na ikiwa jawabu ni ndio : jee atatoa salamu mbili pindi atakapokata Swala ile ama ataikata tu bila ya salamu.
Kamati ikajibu :Sahihi katika kauli mbili za wanazuoni ni kwamba atakata Swala ile , na haihitajiki kwake katika kutoka kwenye ile swala kutoa salamu, na ataungana na imamu moja kwa moja.
Na ALLAH ni mjuzi zaidi.
* Chanzo ni Fatwa ya Sheikh Swaleh Al Munajjid
Na kufanya Tarjam na Ustadh Fadhil Muhammad Al Shiraziy