AR-RAHEEQ AL-MAKHTUM
Wakati watu walipokuwa wakijiandaa kutawanyika baada ya shughuli ya kupeana ahadi na Mkataba Kukamilika, mmoja miongoni mwa Mashetani aliugundua Mkataba huo. Kwa kuwa ugunduzi huo ulikuja wakati wa mwisho na isingewezekana kuwafikishia viongozi wa Makuraishi khabari hii kwa njia ya siri, ghafla wakati wale Waislamu wakiwa bado wamo katika lile bonde, yule Shetani alisimama juu ya kichuguu na kupiga kelele kwa sauti ya juu kabisa ambayo haijawahi kusikika na mtu yeyote! ”Enyi watu mlio majumbani, Je, mtachukua hatua gani dhidi ya Muhammad na watu wengine ambao wameiacha dini yao? Wamekutanika kwa ajili ya kuwapigeni vita.” Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (ﷺ) akasema, ”Huyo ni mtu mbaya sana wa Aqabah, kwa hakika ninaapa kwa Iina Ia Mwenyezi Mungu, Ewe adui wa Mwenyezi Mungu nitaacha mambo yote kwa ajili ya kukushughulikia (kukupiga vita) Kisha akawaamrisha Waislamu kutawanyika na kwenda kwenye kambi zao. (1)
Maandalizi ya Answar Katika Kuwapiga Makuraishi.
Sauti ya shetani iliposikika, Abbasi bin Ubaba bin Nadhlan alisema; ”Ninaapa kwa yule aliyekuleta kwa haki, ukitaka, kesho tutawaendea watu wa Mina kwa panga zetu.” Mtume wa Mwenyezi Mungu (ﷺ) akasema; ”Hatukuamrishwa kufanya hivyo, isipokuwa rejeeni kwenye kambi zenu, wakarejea na kulala mpaka asubuhi. ” (2)
Shutuma za Makuraishi kwa viongozi wa Yathrib
Khabari hii ilipofika katika masikio ya Makuraishi ilizusha mayowe makubwa na kuamsha kero na huzuni, kwa sababu wao walikuwa wanaelewa vizuri athari za mkataba huo na matokeo yake, kuhusiana na nafsi na mali zao. Kulipopambazuka tu tayari ujumbe mkubwa wa viongozi wa Makka na viongozi wa waovu wake ukatoka na kuelekea kwenye kambi ya watu wa Yathrib, kwa lengo la kwenda kutoa malalamiko ya kupinga mkataba huo. Ujumbe huo ulikuwa na ujumbe ufuatao; ”Enyi Jamaa miongoni mwa Khazraji, tumepata khabari kuwa nyinyi mmekuja kwa swahibu yetu huyu kwa nia ya kumchukua kutoka kwetu na mmepeana naye ahadi ya kusaidiana naye katika kutupiga. Na kwa jinsi mambo yalivyo, tunaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu hakuna kabila lolote la Waarabu litakalo chukiza zaidi kwetu, kwa sababu ya kuzuka vita kati yetu na kati yao zaidi ya nyinyi, Kwa vile khabari za mkataba huo zilifanyika kwa siri Sana, Mushirikina wa Khazraji hawakuelewa chochote kuhusiana na mkataba huo na kwa hivyo hawakuwa na uhakika isipokuwa dhana tu ndiyo iliyowafanya wafimke na kuapa ovyo. kuwa hawana uhakika na jambo hilo. Watu hawakufahamu lolote na walilazimika kwenda kwa Abdallah bin Ubay bin Salul kwa matumaini ya kupata khabari, yeye aliwaeleza kwa kusema; ”Khabari hizi siyo za kweli ni batili, jambo hili halikutokea, si rahisi kwa watu wangu kuzua jambo mfano wa hili, laiti ningelikuwepo Yathrib, watu wangu wasingelifanya jambo hilo bila ya kunishauri.”
Waislamu walitazamana tu na kukaa kimya, hakuzungumza mtu yeyote miongoni mwao kwa kukanusha au kuthibitisha khabari hizo. Ama viongozi wa Kikuraishi waliwasadiki Mushirikina wenzao na wakarejea bila ya mafanikio yoyote.
Makuraishi Wanathibitisha Khabari na Kutafutwa Kwa Watoaji Ahadi:
Viongozi wa Makka walirejea wakiwa na imani kwa asilimia kubwa kuwa jambo hili halikufanyika, na kuwa taarifa wanazopata ni za uongo. Hata hivyo wao hawakuacha kupeleleza na kufuatilia mpaka ilipokuja kuthibitika kwao kuwa khabari walizosikia ni sahihi na kuwa Mkataba umekamilika kwa vitendo. Khabari hizi wao walizipata baada ya mahujaji kuanza kuondoka kur‘ejea walikotoka. Haraka haraka wakatuma wapanda farasi wao kuwafuata watu wa Yathrib, baada ya kupita muda walifanikiwa kumwona Sa’ad bin Ubada na Mundhir bin Amri, wakawa wanafukuzana nao, Mundhir aliwashinda na hawakumpata.
Lakini walifanikiwa kumpata Sa’ad wakamkamata na kuifunga mikono yake shingoni mwake kwa kamba ya tandiko la mnyama wake, kisha wakawa wanampiga na kumkokota chini na kuzivuta nywele zake mpaka walipomuingiza Makka. Mut’im bin Adiyy na Al-Harithi bin Harb bin Umayya walikuja na kumtoa kutoka mikononi mwao kwa sababu Sa’ad alikuwa akidhamini usalama wa misafara yao ya biashara inayopita Madina. Ansar wakashauriana pindi walipomkosa Sa’ad, lakini mara akawatokea, wakaendelea na msafara wao mpaka Madina. (3)
Huu ndio mkataba wa Al-Aqaba wa pili, mkataba ambao unajulikana kwa jina la mkataba mkubwa wa Al-Aqaba na ulifanyika katika mazingira yaliyotawaliwa na hisia za ushujaa, kuaminiana, kupendana, kuhurumiana na kusaidiana kati ya Waumini mbalimbali kwa ajili ya Dini. Ikawa Muumini katika watu wa Yathrib anamuonea huruma nduguye Muumini anayedhulumiwa huko Makka. Yuko tayari kumnusuru kwa nguvu zote na anamchukia mwenye kumdhulumu, zinaibuka hisia zake za ndani zilizojaa mapenzi kwa nduguye Muislamu anayeteswa, ambaye anampenda ghaibu katika dhati ya Mwenyezi Mungu (ﷻ).
Hisia hizi hazikuwa ni msukumo wa muda ambao ungeondoka baada ya masiku kadhaa kupita, lakini ukweli ni kuwa chimbuko la mapenzi hayo lilikuwa ni Imani waliyokuwa nayo kwa Mwenyezi Mungu (ﷻ) na Mjumbe Wake (ﷺ) na Kitabu Chake Kitukufu, Imani ambayo haiwezi kuonclolewa na nguvu yoyote. Imani ambayo inapotoka ile hisia yake huzaa na matokeo yake huwa ni kujengeka kwa itikadi yake na utendaji wake kuwa mzuri. Kutokana na Imani hii, Waislamu waliweza kuandika kurasa za zama hizo historia iliyojaa matendo ya kishujaa, na wakaacha athari zilizopo mpaka leo hii, ambazo hazifanani na mifano iliyotangulia wala iliyopo na pengine haitapatikana siku zijazo.