SOMO LA FIQHI
Sheria haikumuachia kila mtu aitekeleze ruhusa hii ya upakazaji maji juu ya khofu kwa namna aitakayo mwenyewe, bali imeelekeza namna maalumu ya upakaji ambayo kila mtu hana budi kuifuata.
Atapukusa juu ya khofu kwa mikono yake miwili ikiwa majimaji, kuanzia kwenye vidole vya miguu yake mpaka kwenye muundi wake mara moja. Atapukusa mguu wakulia kwa mkono wa kulia na mguu wa kushoto kwa mkono wa kushoto.
Wala hapukusi chini ya khofu wala kisiginyo chake. Ali Radhi za Allah ziwe juu yake amesema:
[لَوْ كَانَ الدِّينُ بِالرَّأْيِ لَكَانَ أَسْفَلُ الْخُفِّ أَوْلَى بِالْمَسْحِ مِنْ أَعْلَاهُ، وَقَدْ رَأَيْتُ رَسُولَ اللهِ ﷺ يَمْسَحُ عَلَى ظَاهِرِ خُفَّيْهِ ] رواه أبو داود
[Lau Dini ilikuwa ni kwa maoni ingekuwa kupukusa chini ya khofu ni bora kuliko juu yake. Na kwa hakika nilimuona Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ akipukusa juu ya khofo zake] [Imepokewa na Abu Daud.].
MUDA WA KUPANGUSA KHOFU MBILI:
Usiku na mchana kwa mkazi na siku tatu pamoja na masiku yake kwa msafiri.
Dalili yake ni neno la Ali Radhi za Allah ziwe juu yake Amesea:
[جَعَلَ رَسُولُ اللهِ ﷺ ثَلَاثَةَ أَيَّامٍ وَلَيَالِيَهُنَّ لِلْمُسَافِرِ، وَيَوْمًا وَلَيْلَةً لِلْمُقِيمِ] رواه النسائي
[Mtume amemwekea msafiri siku tatu na masiku yake, na amemwekea mkazi wa mji usiku mmoja na mchana wake] [Imepokewa na An Nasai].
HESABU YA MUDA WA KUPANGUSA
Muda unaanzia mwanzo wa kupangusa baada ya kutangukiwa na udhu. Avaapo soksi mbili akiwa kwenye hali ya utwahara, kisha akaukosa twahara kwa mara ya kwanza, basi kuanzia kupangusa huku kutahesabiwa usiku na mchana (masaa ishirini na nne). Mfano wake ni mtu aliyetawadha, akaosha miguu yake kisha akavaa soksi zake, akaswali alfajiri, na wakati wa saa nne asubuhi alitokewa na vitanguo, na udhu wake ukatanguka. Ilipofika saa tano asubuhi alitawadha na akaswali Dhuha na akapukusa soksi zake. Hapa yafaa kwake yeye kuendelea kuvaa soksi mbili na kupukusa juu yake mpaka saa tano asubuhi ya siku ya pili.
Hayo ni kwa mkazi ama msafiri ni kwa muda wa siku tatu na masiku yake