SOMO LA FIQHI
TunAkusudia kwa ibara (Muda wa hedhi) kile kipindi ambacho mwanamke hutumika yaani huwamo hedhini.
Kipindi hiki tunaweza kukigawa katika sehemu tatu,kama ifuatavyo:-
KIPINDI KIFUPI
Huu ndio muda wa chini kabisa wa kutoka damu ya hedhi hiki ni kipindi cha masaa ishirini na nne (24). Hii inaamaanisha kuwa mwanamke anaweza kuingia hedhini mchana na usiku wake tu, kisha damu ikakatika.
KIPINDI KIREFU
Huu ndio muda wa juu kabisa wa kutoka damu ya hedhi. Hiki ni kipindi cha siku kumi na tano (15), mchana na usiku.
KIPINDI CHA GHALIBU
Huu ndio muda wa ada na desturi kwa wanawake walio wengi, yaani wanawake wengi hutumika katika kipindi hiki. Huu ni muda wa siku sita au saba.
MUDA WA UTWAHARA
Muda wa chini wa twahara, yaani kipindi cha chini ambacho mwanamke anakuwa katika twahara ni siku kumi na tano (15).
Hakuna ukomo (limit) wa wingi wa twahara kwani inawezakana kabisa mwanamke asipate hedhi kwa muda wa mwaka, miaka miwili au miaka kadhaa na hili limethibiti kwa majaribio
Mwanamke atakapoiona damu chini ya kipindi kifupi cha hedhi yaani chini ya masaa ishirini na nne au aliiona damu baada ya kule kipindi kirefu cha hedhi, yaani baada ya siku kumi na tano, damu hii itazingatiwa kisheria kuwa ni damu ya ISTIHAADHA na sio damu ya hedhi.