MAMBO YANAYOPENDEKEZWA KUFANYWA NDANI YA SAUMU
1. Kula daku na kuchelewesha kula daku hadi karibu sana na kuadhiniwa alfajiri
Kwa kauli ya Mtume ﷺ:
[تسحروا فإن في السحور بركة] رواه البخاري ومسلم
[Kuleni daku, hakika katika kula daku kuna Baraka] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]
Na inahesabika kula daku kwa kupatikana chakula kingi au kidogo, hata kama ni tama la maji kwa kauli ya Mtume ﷺ:
[السُّحُورُ أَكْلَةٌ بَرَكَةٌ فَلا تَدَعُوهُ وَلَوْ أَنْ يَجْرَعَ أَحَدُكُمْ جَرْعَةً مِنْ مَاءٍ فَإِنَّ اللَّهَ وَمَلائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى الْمُتَسَحِّرِينَ] رواه أحمد
[Daku uchache wake ni baraka, basi msiache kula daku, hata kama atakunywa mmoja wenu tama la maji, kwani Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanawaswalia wenye kula daku] [Imepokewa na Ahmad.]
Na inapendekezwa kuchelewesha kula daku, kutoka kwa Zaid ibn Thaabit radhi za Allah zimfikie yeye Anasema:
[تَسَحَّرْنَا مَعَ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ثُمَّ قَامَ إِلَى الصَّلَاةِ قُلْتُ كَمْ كَانَ بَيْنَ الْأَذَانِ وَالسَّحُورِ قَالَ قَدْرُ خَمْسِينَ آيَة] رواه البخاري ومسلم
[Tulikula daku pamoja na Mtume ﷺ, kisha tukasimama kuswali (yaani swala ya alfajiri), anasema Anas ibn Malik: nikasema: ilikuwa ni kipindi cha mda gani kati ya kula kwenu hiyo daku na kuswali? Akasema: kiwango cha (kusoma) Aya hamsini)] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]
FAIDA
Kunywa wakati adhana inapo adhiniwa
Mtu anaposikia adhana na kinywaji chake kipo mkononi mwake basi anaruhusiwa kunywa hadi amalize; kutoka kwa Abu Hureirah anasema: Amesema ﷺ:
[إذا سمع أحدكم النداء والإناء على يده فلا يضعه حتى يقضي منه حاجته] رواه أبوداود
[Atakaposikia mmoja wenu adhana na hali ya kuwa chombo cha kunywea maji kipo mkononi mwake basi asikiweke kando mpaka amalize haja yake ya kutumia hicho chombo] [Imepokewa na Abuu Daud.]
Na wanazuoni wamesema kuhusu hadithi hii ni kwa Yule ambae ana shaka kutokeza kwa alfajiri, ama akihakikisha kuwa alfajiri imetokeza kwa huyu hafai kuendelea kula wala kunywa, na akiendelea kufanya hivyo Saumu yake imebatilika na itamlazimu Ailipe
2. Kufanya haraka katika kufungua saumu.
Yapendekezwa kwa aliyefunga kufanya haraka kufungua saumu yake pindi tu anapohakikisha kwamba jua limezama na kuingia jioni.; kwa kauli ya Mtume ﷺ:
[لا يَزَالُ النَّاسُ بِخَيْرٍ مَا عَجَّلُوا الْفِطْر] رواه البخاري ومسلم
[Watu wangali katika kheri pindi wanapoharakisha kufungua saumu zao.] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]
FAIDA
Na inapendekezwa mtu kufungua saumu kwa rutab (tende tosa), asipopata rutab basi afungue kwa tende, na hizo tende ziwe ni hesabu isiyogawanyika kwa mbili (kama vile tende moja, tatu, tano na mfano huu), asipopata tende basi na anywe matama ya maji; kulingana na hadithi ya Anas ibn Malik, anasema: “Alikuwa Mtume ﷺ anafungua saumu kwa Rutab (Tende Tosa) kabla hajaswali, na ikiwa hakuna Rutab basi alikuwa akifungua kwa tende kidogo hivi, na ikiwa hakuna tende alikuwa akinywa [ Hasaa: alikunywa.] matama ya maji” [Imepokewa na Tirmidhi.].
Na akiwa hakupata kitu chochote cha kufungulia saumu basi atanuia kufungua saumu kwa moyo wake, na hili litamtosheleza kwamba amefungua.
MAS’ALA
Atakae Funguwa kwa bahati mbaya
Atakapo kula mtu aliyefunga hali ya kudhania kwamba jua limezama na kuingia jioni, au kwa kutoelewa kutokeza kwa alfajiri, kisha ije kum’bainikia kinyume na alivyodhania, basi haimlazimu kwake kuilipa saumu hiyo; kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukfu:
{لَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ فِيمَا أَخْطَأْتُم بِهِ وَلَٰكِن مَّا تَعَمَّدَتْ قُلُوبُكُمْ} الأحزاب5
[Wala si lawama juu yenu mkikosa, lakini (kuna lawama) katika yale ziliyoyafanya nyoyo zenu kwa kusudi ] [ Al-Ahzab- Aya 5]
Na kauli yake Mtume ﷺ:
[إن الله تـجاوز لي عن أمتي الـخطأ والنسيان وما استكرهوا عليه] رواه إبن ماجة والبيهقي
[Hakika ya Mwenyezi Mungu amewaondoshea umma wangu (hawaandikiwi madhambi) kwa jambo watakalolikosea bila ya kukusudia na kwa watakayofanya kwa kusahau, na kwa watakayolazimishwa kufanya] (hali ya kuwa wao wenyewe wanayachukia)” [ Imepokewa na Ibnu Maajah na Al Bayhaqiy.]
3. Kuomba Dua wakati wakufungua saumu.
Kwa ilivyo Thubutu kutoka kwa Mtume ﷺ Alipokuwa akifunguwa Saumu Akisema:
[ذَهَبَ الظَّمَأُ وَابْتَلَّتْ الْعُرُوقُ وَثَبَتَ الْأَجْرُ إِنْ شَاءَ اللَّهُ] رواه أبوداود
Na amesema Mtume ﷺ:
[للصائمِ عند فِطْرِهِ دَعْوَةً ما تُرَدُّ] رواه إبن ماجة
[Hakika kwa aliyefunga saumu wakati anapofungua kuna dua isiyorudi] [ Imepokewa na Ibnu Maajah.] yaani dua inayokubalika moja kwa moja mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
4. Kuacha mambo ya upuzi na mambo machafu.
Kwa kauli ya Mtume ﷺ:
[إذا كان يوم صوم احدكم فلا يرفث ولا يصخب وإن قاتله أو سابه احد فليقل إني امرؤ صائم] رواه البخاري ومسلم
[Ikiwa ni siku ambayo mmoja wenu amefunga, basi asifanye mambo machafu, [ Yarfuth Kufanya mambo machafu: yatokamana na neno uchafu, nako ni kutamka matamshi mabaya, na vile vile hutumika neno hili kumaanisha tendo la ndoa na vitangulizi vya tendo hili.] wala asikemee wenziwe[ Yaskhab: Yuwakemea: yatokamana na neno kemea, nako ni kubishana na kupiga ukulele.], anapotukanwa na mtu, au anapopigwa vita basi na aseme: Mimi ni mtu niliyefunga] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].
Na kwa neno lake Mtume ﷺ:
[مَنْ لَمْ يَدَعْ قَوْلَ الزُّورِ وَالْعَمَلَ بِهِ فَلَيْسَ لِلَّهِ حَاجَةٌ فِي أَنْ يَدَعَ طَعَامَهُ وَشَرَابَهُ] رواه البخاري
[Asie acha maneno machafu na kuyatumia basi Mwenyezi Mungu hana haja kwa mtu huyo kuacha chakula chake na kinywaji chake] [Imepokewa na Bukhari.]
5. Kuzidisha kufanya Ibada kwa wingi.
Kama kusoma Qur’an, na kufanya adhkari kumtaja Mwenyezi Mungu, na kuswali swala ya Tarawehe, na visimamo vya usiku wakati watu wamelala, na kufanya visimamo vya usiku wa Lailatul Qadri, na kuswali swala za sunnah, na kutoa sadaka, na kuwa mkarimu na kujitahidi katika kufanya mambo ya kheri, na kuwalisha waliofunga wakati wa kufungua saumu zao, na kwenda Umrah, kwasababu matendo mema siku ya Ramadhani malipo yake yanaongezeka mara nyingi sana, kutoka kwa Ibn Abbas anasema:
كَانَ رَسُولُ اللَّهِ -صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ -اجود الناس وَكَانَ اجود مَا يَكُونُ فِي رَمَضَانَ حِينَ يَلْقَاهُ جِبْرِيلُ، وَكَانَ يَلْقَاهُ فِي كُلِّ لَيْلَةٍ مِنْ رَمَضَانَ فَيُدَارِسُهُ الْقُرْانَ، فَلَرَسُولُ اللَّهِ -صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ -اجود بِالْخَيْرِ مِنْ الرِّيحِ الْمُرْسَلَةِ. رواه البخاري
[Alikuwa Mtume ﷺ ni mkarimu kushinda watu wote, na alikuwa mkarimu zaidi wakati wa Ramadhani pindi anapokutana na Jibril, na alikuwa Jibril akikutana na Mtume kila usiku wa mwezi wa Ramadhani, ikawa anamfundisha Qur’ani , basi Mtume ﷺ pindi anapokutana na Jibril alikuwa mkarimu katika mambo ya kheri kushinda upepo mkali uliotumwa.] [Imwpokewa na Bukhari.].
6. Kujitahidi kwa Ibada hasa kumi lamwisho katika Mwezi wa Ramadhani
Imepokewa na bibi A’isha radhi za Allah ziwe juu yake Amesema:
[كان النبي إذا دخل العشر شد مئزره، وأحيا ليله، وأيقظ أهله] رواه البخاري ومسلم
[Alikuwa Mtume ﷺ likingia kumi la mwisho akijifunga kibobwe [(Shadda mi’zarah) Nikinaya cha mtu kujitihidi katika ibada zaidi kuliko ilivo zowewa. Na kumesemwa ni kinaya cha mtu kujiepusha na mkewe, na akiuhuisha usiku na akiwamsha wakezake] [Imwpokewa na Bukhari na Muslim.] akiwatanabahisha kwa ajili ya ibaada na akiwahimiza juu yake.