0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

MALENGO YA TARBIYA- Sheikh Abuu Hamza

MALENGO YA TARBIYA

Sifa njema zote ni za mwenyezi Mungu bwana wa viumbe vyote.Mola aliye nyanyua mbingu saba bila nguzo.Swala na amani zimiminikie mtukufu wa daraja mtume Muhammad ﷺ. Mtume ambaye amekuwa kielelezo na mfano mzuri wa kuigwa kwa tabia nzuri. Mtume aliyetumilizwa kuja kukamilisha akhlaq njema.
Asili ya makala haya ni ndugu yangu Sheikh Said Abdou aliyewasiliana nami na akaniomba niwe nachangia katika kutoa mwongozo katika mada ya malezi mazuri ya watoto wetu kwani mtoto mwenye tarbia nzuri ndiye msingi mzuri wa jamii siku za usoni. Vilevile ukizingatia kuwa pia sisi bado tunahitaji mwongozo katika maisha yetu.
Silsila hii au msururu wa makala haya ’Mwongozo wa Malezi’ makusudio na malengo ni kuweka dira ya kutoka katika malezi ya kubahatisha,kufanya wanaofanya watu na kuelekea katika mwongozo wa sawa katika malezi.
Na ili hili lipatikane,naomba kila mzazi anayefaidika na msururu huu kwanza anifamishe.

Pili ampashe habari mzazi mwenzake juu ya mtandao huu na faida alizopata baada ya kusoma makala haya.Na pia aniombee Mola aniwezeshe kudumu katika kuandika makala haya na yawe yenye kuleta mabadiliko katika jamii.

UMUHIMU WA MALEZI

Malezi ni msingi wa jamii yeyote.Jamii ikitaka kupiga hatua na kuwa na maendeleo ni sharti izingatie malezi bora.Pasi na malezi mazuri yenye lengo na shabaha hakutakuwa na maendeleo,kwa hivyo kuna dharura kubwa sana ya jamii kuzingatia suala la malezi.Kuna haja ya sisi kulea watoto na nafsi zetu katika misingi ya sawa.Ndio tunapata katika Qur’an imeanza na tazkiya ya nafsi ya ndani inayoletwa na malezi mazuri.Katika Suratul Jumuah,aya ya pili,ALLAH (SWT) ameanza na tazkiya ya kusafisha dhamira ya ndani ambayo ni kazi ya tarbia kisha ikatajwa elimu na hekima.

{هُوَ الَّذِي بَعَثَ فِي الْأُمِّيِّينَ رَسُولًا مِّنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِهِ وَيُزَكِّيهِمْ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَإِن كَانُوا مِن قَبْلُ لَفِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ}

[Yeye ndiye aliye mpeleka Mtume kwenye watu wasio jua kusoma, awasomee Aya zake na awatakase, na awafunze Kitabu na hikima, ijapo kuwa kabla ya haya walikuwa katika upotofu ulio dhaahiri.]        [Al-Jumu”:2]

Kwa sababu hii ni wazi kuwa malezi ndio muhimu.
Kama hujui malengo ya kumlea mtoto wako basi ufahamu uko katika hasara kubwa sana.

Malengo ya ulezi hayaanzi baada ya kuzaa mtoto bali pale ulipoanza kufikiria kutafuta baba au mama wa watoto wako.Hapo ndipo palipoanzia malengo ya ulezi.Hii ni kwa sababu athari za wazazi wawili ni muhimu sana katika malezi ya watoto.

NI MALENGO GANI YA MALEZI TUNAYOFAA TUWE NAYO ?

1. Tuwe na malengo ya kuwezesha watoto wetu wamuamini ALLAH (SWT) ,malaika wake,vitabu vyake,mitume yake,kuiamini siku ya hesabu na kuiamini Qadar ya ALLAH (SWT) kheri yake na shari yake.

2. Tuwe na malengo ya kujenga tabia nzuri kwanza kabla ya chochote,kabla hata elimu ya kimaarifa kwani mtu anapokuwa na adabu njema inamrahisishia yeye kupata elimu.

3. Tuwe na malengo ya kuwapa watoto wetu msingi mzuri wa dini na hii inahusisha kumshurutisha mtoto wako ahifadhi Qur’an tukufu kwanza kabla ya kupata maarifa yeyote.Jambo hili la kuhifadhisha watoto Qur’an wakiwa wangali ni wadogo lilipoachwa,likatupelekea kuwa nyuma katika mambo yote.Lakini ikumbukwe kuwa historia ya maulamaa wa kiislamu wa zamani na maajabu waliyoyafanya yote yanahusishwa na wao kuhifadhi Qur’an wangali wadogo.

4. Kisha tuwe na malengo ya kuwafunza watoto wetu lugha ya kiarabu.Lugha ya Qur’an na ya mtume ﷺ lugha ya uislamu.Na wajifakhiri kwayo.Baada ya hapo tuwafunze mambo ya dharura na muhimu ya dini,mfano Tawhid na Fiqh na namna ya kutekeleza ibada na miamala baina ya watu.

5. Vilevile tuwe na malengo ya kuwafunza watoto wetu kujitolea katika kutumikia jamii kihali na mali.Tuwajuze kuwa dini ya uislamu imepiga hatua ya kutufikia sisi kwa sababu ya kujitolea kwa maswahaba na waliowafuata kwa kila njia.Na kujitolea huku kuhusishwe na kutaka radhi za ALLAH (SWT) na sio malipo ya watu au kusifiwa.

6. Pia tuwe na malengo ya kulea watoto wetu kifikra.Tuweze kujenga uwezo wa kufikiria na kubuni mambo yatakayokuwa na manufaa nao.Watoto wetu waweze kufikiria na kuja na masuluhisho ya kwanza na ya haraka wakati wanapatikana na matatizo hata kama mzazi wake hayupo karibu.Kwa hivyo kuna dharura katika madaaris zetu na ndaki zingine za elimu kujumuisha katika mitaala yao namna ya kufikiria.

7. Hata hivyo,inatupasa tuwe na malengo ya kukuza hisia za kuongoza katika vijana wetu.Wanapokua waweze kufikiria namna watakavyoongoza asasi tofauti katika jamii na jinsi gani wanaweza kuja na masuluhisho ya matatizo wanayoyapata waislamu na jamii kwa jumla.Hili likipatikana vijana wetu wataweza kuziba pengo la uongozi liliko hivi sasa.

8. Tena tuwe na malengo ya kuwawezesha vijana wetu wa kiume kubeba majukumu ya kifamilia ndani ya majumba yetu.Hili litawezesha kuchukua hatamu za uongozi ndani ya nyumba iwapo baba hayupo.Jambo hili vilevile litakomaza akili za vijana wetu na kuwafanya wajione watu muhimu hivyo basi kujiheshimu.Na kwa watoto wa kike nao wafunzwe kuwa watiifu na wenye heshima katika majumba.

9. Ni muhimu kuwa na malengo ya kuwafanya vijana wetu wapende fikra ya kuwa na umoja na mshikamano katika umma na kujiepusha na fikra ya mipasuko na migawanyiko kwani yatupasa tuelewe kuwa umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.

10. Hatimaye tuwahimize vijana wetu waweke malengo katika maisha yao.Jambo hili litawasaidia kufanyia kazi hatua zitakazo wafikisha kwenye malengo yao.Utendakazi utaboreshwa hivyo basi uvivu hautakuwa sehemu ya jamii zetu.

Itaendelea katika makala yajayo…

Sheikh Abuu Hamza

Mombasa -Kenya

Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.