KWA BANU SA’AD
Siku hizo ilikuwa ni mazoea ya watu wa mijini katika Waarabu kuwatafutia watoto wao wanyonyeshaji wa mashambani ili kuwaepusha watoto wao na magonjwa ya mijini, ill iwe na nguvu miili yao, ikazane mishipa yao na waweze kukisema Kiarabu fasaha katika utoto wao.Abdul Muttwalib akamtafutia Mjumbe wa Mwenyezi Mungu ﷺ wanyonyeshaji. Alimtaka mwanamke mmoja kutoka katika ukoo wa Saad bin Bakri, Halima binti Abi Dhuayb amnyonyeshe Mtume.Mume wa bibi huyu alikuwa ni Al- Harithi bin Abdil-Uzaa aliyekuwa akijulikana kwa jina la Abi Kabshah kutoka katika kabila hilo hilo.
Ndugu zake Mtume ﷺ wa kunyonya kutoka kwa mama huyo ni, Abdallah bin Al-Harithi, Unaysah binti Al- Harithi Hadhafa au Sudhamah binti Al-Harithi (na huyu ndiye Al-Shaymaa na hili ndilo jina lililoeleweka zaidi mijini kuliko hata jina lake halisi) naye alikuwa ni mmoja kati ya waliokuwa wakimlea Mjumbe wa Mwenyezi Mungu ﷺ na Abu Sufyan bin Al-Harithi Bin Abdul Muttwalib, mtoto wa Ammi ya Mtume ﷺ.
Ammi ya Mtume ﷺ Hamza Bin Abdul Muttwalib alikuwa amenyonyeshwa kwa Banu Saad bin Bakri, mama yake alimnyonyesha Mjumbe wa Mwenyezi Mungu ﷺ siku moja wakati akiwa kwa mama yake Halima. Kwa hivyo,Hamza alikuwa ni mshirika na Mjumbe wa Mwenyezi Mungu katika kunyonya kwa sehemu mbili, sehemu ya Thuwayba na sehemu ya Al-Saadiyya.