0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

KUTOKA NYUMBANI KWENDA PANGONI


AR-RAHEEQ AL-MAKHTUM


Mtume wa Mwenyezi Mungu (), aliondoka nyumbani kwake katika usiku wa tarehe 27, Safar, katika Mwaka wa kumi na Nne wa Utume wake, muafaka na 12 .622 C.E.,  (1) kwenda nyumbani kwa rafiki yake, Abubakar (Radhi za Allah ziwe juu yake ), na kisha wakaiacha nyumba ya Abubakar (Radhi za Allah ziwe juu yake ), kupitia mlango wa nyuma ili watoke Makka haraka kabla ya kuchomoza alfajiri.

Mtume (), alielewa kuwa Makuraishi watamtafuta sana na kuwa njia ambayo wataifuata watafutaji kwanza itakuwa ni njia kuu ya kuelekea Madina, kwa upande wa Kaskazini. Kulijua hilo Mtume ‘(), alipita njia tofauti kabisa na hiyo, yeye aliifuata njia inayotoka Kusini mwa Makka inayoelekea upande wa Yemen. Aliifuata njia hii kiasi cha maili tano mpaka akafika kwenye Jabali refu sana, kuna ugumu katika kupanda kwake. Mtume (), alilipanda bila ya viatu na huenda ilifanywa hivyo makusudi na Mtume (), ili afiche nyayo zake.

Mtume (), alipofika juu ya jabali alibebwa na Abubakar (Radhi za Allah ziwe juu yake ) na kumpeleka hadi pangoni, pango lenye kufahamika katika historia kama pango la Thaur. (2)

Wakati wakiwa Pangoni

Walipofika kwenye pango Abubakar (Radhi za Allah ziwe juu yake ) alisema; “Ninakuomba kwa jina la Mwenyezi Mungu (ﷻ) usiingie pango hili mpaka niingie mimi kwanza, ili kama kutakuwemo na kitu kibaya usiathirike.” Akaingia pangoni na kusafisha vema mle ndani, pembezoni mwa kuta zake alikuta matundu matatu, alipasua shuka yake akaziba kwa shuka hiyo moja kati ya yale matundu matatu, na matundu yale mengine akayaziba kwa kutumia miguu yake na Kisha akamwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu () aingie, akaingia na kujilaza kwa kupumzika huku kichwa chake amekiegemeza mapajani mwa Abubakar (Radhi za Allah ziwe juu yake ) ya mto. Akiwa Katika hali hiyo Abubakar (Radhi za Allah ziwe juu yake ) aliumwa na mdudu, mwenye sumu, katika mmoja wa miguu yake aliyoitumia kuziba yale matundu, hakutikisika kwa kuogopa kumuamsha Mtume wa Mwenyezi Mungu (). Kwa uchungu wa kuumwa kwake akawa anabubujikwa na machozi yaliyodondoka katika uso wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (). Akashituka na kuhoji, “Una nini ewe Abubakar’?.” Abubakar (Radhi za Allah ziwe juu yake ) akajibu na kusema, “Nimeumwa  na mdudu na nina maumivu makali.” Kusikia hivyo Mjumbe wa Mwenyezi Mungu () akatemea mate pale alipoumwa. Mara maumivu yote aliyokuwa nayo yakatoweka. (3)

Walijificha ndani ya pango kwa muda wa siku tatu, usiku wa Ijumaa na Jumamosi na Jumapili. (4)

Wakati woté huo Abdillah bin Abubakar (Radhi za Allah ziwe juu yake ) ndiye aliyekuwa akilala pamoja nao; Aisha (Radhi za Allah ziwe juu yake ) anasema, “Abdillah ni kijana mwenye fahamu nzuri, mwepesi wa kujifunzamambo na mwepesi wa kuelewa. Alikuwa anaondoka usiku mwingi, na kunapopambazuka tayari huwa yuko na Makuraishi Makka kama vile mtu aliyelala pale. Alikuwa akiwaletea khabari zote za vitimbi na njama walizokuwa wakizipanga Makuraishi wakati kiza kinapoanza.

Mchungaji wa mbuzi wa maziwa wa Abubakar (Radhi za Allah ziwe juu yake ) , Amir bin Fuhaira, aliyekuwa huru wake, ndiye aliyekuwa akiwapitishia maziwa wakati wa jioni. Hicho ndicho chakula walichokuwa wakilalia. Amir bin Fuhaira, alifanya hivyo mfululizo kwa muda wa siku zote tatu, (5) na alikuwa akiwapitisha mbuzi kwenye nyayo za Abdillah bin Abubakar wakati wa kurudi kwake Makka, alikuwa akifanya hivyo kwa lengo la kufuta nyayo zake

Makuraishi walipandwa na hasira walipobaini kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu () aliwaponyoka pamoja na Abubakar (Radhi za Allah ziwe juu yake ) usiku wa siku waliyodhamiria kutekeleza mpango wa kumwua.

Jambo la kwanza walilofanya kuhusu tukio hili, walimpiga Ali (Radhi za Allah ziwe juu yake ), wakamkokota mpaka kwenye Al-Ka’aba, wakamfunga kwa muda wa saa moja kwa matmunaini kuwa huenda akatoa khabari za alikokwenda Mtume (). Baada ya kushindwa kupata khabari kutoka kwa Ali (Radhi za Allah ziwe juu yake ), walikwenda nyumbani kwa Abubakar (Radhi za Allah ziwe juu yake ) na kugonga mlango wake, Asmaa binti Abubakar (Radhi za Allah ziwe juu yake ) alitoka na wakamwuliza, ”Yu wapi ‘baba yako?.” Akasema, “’Sielewi.” Walipokuwa mlangoni, Abu Jahli alimpiga makofi kwa nguvu shavuni mpaka hereni zake zikakatika. (6)

Makuraishi waliamua katika kikao cha dharura kutumia njia zote ambazo zitawawezesha kuwakamata watu wawili hao. Wakaziweka njia zote Zenye kupitika kutoka Makka, chini ya uangalizi mkali wa askari katika pande zote, kama ambavyo walikubaliana. Waliamua kumpa malipo makubwa, kiasi cha ngamia mia moja, ambaye atawafikisha kwa Makureish wakiwa hai au maiti (7)

Juhudi za kuwatafuta zilianza, wapanda farasi, waenda kwa miguu na wafuatiliaji wa athari za nyayo wakawa wanawatafuta kwenye majabali, majangwa, mabonde na vichuguu, lakini hawakufanikiwa. Walifika mpaka kwenye mlango wa pango alipojificha Mtume (). na Abubakar (Radhi za Allah ziwe juu yake ).

Bukhari amepokea kutoka kwa Anas (Radhi za Allah ziwe juu yake ) aliyepokea kutoka kwa Abubakar (Radhi za Allah ziwe juu yake ); Amesema: Nilikuwa pamoja na Mtume () ndani ya pango nikanyanyua kichwa changu na ghafla nikaziona nyayo za watu, nikasema, “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu laiti- baadhi yao wangeinamisha vichwa vyao wangetuona.” Akasema; “Nyamaza ewe Abubakar, sisi tu watu wawili ambao Mwenyezi Mungu ni watatu wetu.” Na katika tamko lingine, ”Nini dhana yako ewe Abubakar kwa wawili ambao watatu wao ni Mwenyezi Mungu. “ (8)

Kwa hakika jambo hilo lilikuwa ni muujiza ambao Mwenyezi Mungu (ﷻ) Alikuwa Amemkirimu Mtume (). kwani walirejea watafutaji wakati ambapo hazikubbaki kati yano na mapango isipokuwa hatua chache sana zene kuhisabika.


1) Mwezi huu wa Safar wa mwaka wa kumi na nne baada ya kupewa Utume kama tutakubaliana mwanzo wa mwaka unaoanzia Muhnrrnm. Lakini kama mwanzo wa mwaka utaanzia ule mwezi ambao Mwenyezi Mungu Alimkirimu Utume Mtume wake, basi mwezi huu wa S_afar utakuwa ni wa mwaka wa kumi na tatu wengi wanaoandika vitabu vya Sira huchagua hili la pili. Hili ndilo linalowachanganya wengi katika kuorodhesha matukio ya kihistoria. Kwa ajili hiyo ndio maana sisi tukaanzka kwa mwezi wa Muharram
2) Rahmatun Lil ‘Alamin, Iuzuu 1, Uk. 95. Mukhtasar Sira, Uk. 197. 294
3) Razin amepokea kutoka kwa ’Umar bin Khattab (r.a). (Angalia, Mishkatil Masabih, juzuu 2, Uk. 556.)
4) Fathul Bari, Iuzuu 7, Uk. 336. 295
5) Sahihil Bukhari, Juzuu 1, Uk. 553, 554.
6) lbn Hisham, Iuzuu 1, Uk. 486.
7) Sahihil Bukhari, juzuu 1, Uk. 554
8) Sahihil Bukhari, Iuzuu 1, Uk. 516, 558. 

Begin typing your search above and press return to search.