KUJILA ZIMISHA NA SUNNAH
Shukrani za dhati ni za Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala Bwana wa viumbe vyote. Na rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad. Swalla Llahu Alayhi wasallam.
Ni nani kati yetu ambaye hapendi apendwe na Mtume ﷺ ?
Ni nani kati yetu ambaye hampendi Mtume ﷺ ?
Ni nani kati yetu ambaye hatarajii kuwa pamoja na Mtume ﷺ ?
Ni nani kati yetu ambaye hatarajii maombezi ya Mtume ﷺ ?
Jawabu ni kuwa hakuna mtu asiyetaka yote tuliyoyataja. Na njia ya pekee ya kutufikisha kumpenda yeye ni kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu(Subhaanahu wa Taala). Na miongoni mwa alama za mapenzi ya kweli ya kumpenda Mtume ﷺ ni kumtii na kufuata Sunna zake. Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala amesema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا النساء:59
[Enyi mlio amini! Mt’iini Mwenyezi Mungu, na mt’iini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema.] [Al-Nnisaa: 59]
Pia amesema Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala:
{قُلْ أَطِيعُوا اللَّهَ وَالرَّسُولَ ۖ فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّ اللَّهَ لَا يُحِبُّ الْكَافِرِينَ} آل عمران:32
[Sema: Mt’iini Mwenyezi Mungu na Mtume. Na wakigeuka basi Mwenyezi Mungu hawapendi makafiri.] [Al-Imraan:32]
Katika aya nyingine Amesema tena Mola: Subhaanahu wa Taala:
{مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّهَ ۖ وَمَن تَوَلَّىٰ فَمَا أَرْسَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ حَفِيظًا} النساء:80
[Mwenye kumt’ii Mtume basi ndio amemt’ii Mwenyezi Mungu. Na anaye kengeuka, basi Sisi hatukukutuma wewe uwe ni mlinzi wao] [Al-Nnisaa:80]
Na ziko Aya nyingi zenye maana kama haya lakini tulizozitaja zinatosha.
Na Mtume ﷺ , alituhimiza sana kumtii yeye katika hadithi nyingi sana. Miongoni mwa hadithi hizo; Mtume ﷺ amesema:
أوصيكم بتقوى الله عز وجل، والسمع والطاعة، وإن تأمر عليكم عبدٌ؛ فإنه من يعش منكم فسيرى اختلافًا كثيرًا، فعليكم بسنتي وسنة الخلفاء الراشدين المهديين، عَضُّوا عليها بالنواجذ، وإياكم ومحدثات الأمور؛ فإن كل بدعةٍ ضلالةٌ رواه أبوداود والترمذي
[Nawausia uchaji Mwenyezi Mungu na kusikiliza na kutii na hata akiwa kiongozi wenu ni mtumwa. Na atakayeishi katika nyinyi ataona tofauti nyingi, basi shikamaneni na Sunna yangu na Sunna ya makhalifa wema waongofu, ishikeni kwa magego] [Imepokewa na Abuu Daud na Al-Tirmidhiy]
Pia Mtume ﷺ tena:
[كل أمتي يدخلون الجنة إلا من أبى، قيل يا رسول الله، ومن يأبى؟ قال: من أطاعني دخل الجنة، ومن عصاني فقد أبى] رواه البخاري
[Umma wote utaingia peponi isipokuwa atakayekataa kuingia peponi. Maswahaba wakamuuliza: Ni nani atakayekataa ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema Mtume Atakaye nitii mimi ataingia peponi na atakayeniasi basi atakuwa amekataa] [Imepokewa na Bukhari]
Katika maneno ya maswahaba juu ya kushikamana na Sunna. Amesema Umar Ibn Khatwab Radhi za Allah ziwe juu yake alipokuwa akilibusu Hajar Aswad (jiwe jeusi):
[إنِّي لأَعْلَمُ أَنَّك حَجَرٌ , لا تَضُرُّ وَلا تَنْفَعُ , وَلَوْلا أَنِّي رَأَيْتُ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم يُقَبِّلُكَ مَا قَبَّلْتُكَ]
[Hakika mimi najua wewe ni jiwe hunufaishi wala hudhuru, na lau nisingelimuona Mtume akikubusu basi nisingelikubusu.]
Ndugu katika imani! Ningependa kuwatajia faida anazopata Muislamu endapo atashikamana na Sunna za Bwana Mtume ﷺ Na miongoni mwa faida hizo ni kama zifuatavyo:
FAIDA YA KUSHIKAMANA NA SUNNAH
1. Kushikamana na Sunna ni kinga na hifadhi ya Waislamu wasifarikiane kwani ndiyo ambayo huleta mshikamano baina ya waumini na kuwa watu hawafarakani madamu watashikamana kwao na Sunna ya Bwana Mtume rehma na amani zimfikie.
2. Faida ya pili ya kushikamana na sunna ni kuokoka na kipote kipotofu kitakacho kwenda motoni. Amesema Mtume ﷺ :
[Jua ya kwamba waliokuwa kabla yenu waliopewa kitabu waligawanyika mapote sabini na mbili, na umma huu utagawanyika vipote sabini na tatu, vipote sabini na mbili vitaenda motoni na kimoja pekee ndicho kitakachoenda peponi nacho ni kinachoshikamana na Sunna]
3. Faida nyengine ya kushikamana na Sunna ni kupata uongofu na kusalimika na upotofu. Amesema ﷺ :
[Enyi watu, hakika mimi nimewaachia kitu mutakaposhikamana nacho hamtapotea milele: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu.] Kwani kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Bwana Mtume Swalla Llahu ‘alayhi wasallam vinamuongoza aliyeshikamana navyo.
4. Miongoni mwa faida za kushikamana na sunna ni kwamba mtu atakaposhikamana na Sunna ataingia katika kundi la Mtume ﷺ. Anahadithia Anas Ibn Malik Mwenyezi Mungu awe radhi naye, ya kwamba walikuja watu watatu katika nyumba za Mtume ﷺ. Wakaulizia ibada ya Mtume ﷺ. Wakaelezewa ibada yake basi waliiona kidogo sana. Wa kwanza akasema: Mimi nitaswali usiku kucha milele wala sitolala. Wa pili akasema : Mimi nitafunga siku zote na wala sitokula hata siku moja. Wa tatu akasema: Mimi nitajiepusha na wanawake milele sitaoa. Alipokuja Mtume ﷺ akaelezewa kuhusu maswahaba wale akawaambia:
أنتم الذين قلتم كذا وكذا؟ أما والله إني لأخشاكم لله وأتقاكم له، لكني أصوم وأفطر، وأصلي وأرقد، وأتزوج النساء، فمن رغب عن سنتي فليس مني
[Nyinyi ndio mliosema hivi na hivi na hivi? Ama mimi naapa kwa Mwenyezi Mungu ya kwamba mimi ni mchaji Mwenyezi Mungu zaidi pamoja na hivyo, mimi naswali usiku nalala nafunga na siku nyingine nala na vile vile naoa wanawake. Basi anayejiepusha na mwenendo wangu si katika mimi]. [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
HUKMU YA KUIWACHA SUNNAH
Na kujiepusha na Sunna ya Mtume inaweza kuwa maasi au ni ukafiri, tunamuomba Mwenyezi Mungu atulinde na ukafiri. Mtu atakapoacha Sunna kwa kuipuuza na kuipinga na kuikosoa atakuwa ameikosoa Dini na kuikosoa Dini ni katika sampuli za ukafiri.Tunajilinda kwa Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala na ukafiri.
Na endapo mtu ataacha Sunna kwa uvivu, sio kwa njia ya kuikosoa basi ni kulingamana na Sunna yenyewe, ikiwa ni jambo la wajibu, atapata dhambi kwa kuacha wajibu na akiacha lililopendekezwa atakuwa amepitwa na fadhila kubwa kabisa.
Kwa hivyo ni juu yetu kushikamana na Sunna za Bwana Mtume ili tupate radhizake Mwenyezi mugnu Mtukufu.
SIKILIZA MADA HII NA SHEIKH ALI BAHERO