NI IPI ITIKADI YA MASHIA KUHUSU NDOA YA MUT’AH NA INA UBORA GANI KWAO?
Ndoa ya Mut’ah ina fadhila kubwa kwa Raafidhwah, kama wanavyodai. Imekuja katika kitabu ‘Manhajus-Swaadiqiyn’ cha Fat-hullaah Al-Kaashaan, kapokea toka kwa Asw-Swaadiq: “Hakika Mut’ah ni katika dini yangu na dini ya baba yangu, basi mwenye kuifanya hiyo anatekeleza dini yetu, na mwenye kuipinga, huyo atakuwa anaipinga dini yetu, bali huyo anaifuata dini nyingine isiyokuwa dini yetu, na mtoto anaezaliwa katika ndoa ya mut’ah ni bora kuliko anayezaliwa katika ndoa ya kawaida, na mwenye kuipinga mut’ah huyo ni kafiri ameritadi.”(1)
Amenukuu Al-Qummiy katika kitabu ‘Man Laa Yahdhwuruhul-Faqiyh’ kutoka kwa ´Abdullaah bin Sinaaniy, kutoka kwa ´Abdullaah amesema: “Hakika Allaah Mtukufu Katuharamishia kinywaji chochote chenye kulevya, na akatupa badala yake Mut’ah.”(2)
Na imekuja katika ‘Tafsiyr Manhajis-Swaadiqiyn’ ya Mullaa Fat-hullaah AlKaashaaniy: “Amesema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), mwenye kufanya mut’ah mara moja, basi huachwa huru na moto theluthi yake, na mwenye kufanya mara mbili huachwa huru na moto theluthi mbili, na mwenye kufanya mara tatu, basi huachwa huru na moto yeye mzima.”
Na katika kitabu hicho hicho, imekuja kuwa “Kasema Mtume (ﷺ), mwenye kufanya mut’ah mara moja, basi huyo kasalimika na ghadhabu za Allaah, na atakayefanya mara mbili atafufuliwa pamoja na watu wema, na atakayefanya mara tatu huyo atakuwa nami peponi.”
Pia katika kitabu hicho hicho kwamba amesema Mtume (ﷺ), mwenye kufanya mut’ah mara moja, anakuwa katika daraja ya Husayn, na mwenye kufanya mut’ah mara mbili yuko katika daraja ya Hassayn, na mwenye kufanya mut’ah mara tatu, anakuwa katika daraja ya ´Aliy bin Abi Twaalib, na mwenye kufanya mara nne daraja yake ni kama daraja yangu,”(3)
Na Marafidhwah hawakuainisha idadi maalumu katika suala la mut’ah, imekuja katika ‘Furuw’ul-Kaafiy’ na ‘At-Tahdhiyb’ na ‘Al-Istibswaar’ kutoka kwa Zuraarah kapokeya toka kwa Abu ´Abdillaah, kasema: “Aliulizwa kuhusu mut’ah kwamba je ni katika wanawake wanne walioruhusiwa? Akasema: Waweza kuoa mpaka elfu moja, kwa sababu wao ni wenye kukodiwa.
Na pia imepokewa kutoka kwa Muhammad bin Muslim, kutoka kwa Abu Ja’afar kwamba, alisema kuhusu ndoa ya mut’ah: Kwamba hao si katika wale wanne, kwa sababu mwanamke anayeolewa ndoa ya mut’ah hapewi talaka, wala hana fungu lolote katika mirathi, bali yeye ni mwenye kukodiwa tu.”(66) Vipi hali hii na ilihali Allaah Anasema:
“Na wale ambao tupu zao wanazilinda. Isipokua kwa wake zao au kwa (wanawake) wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, basi hao ndio wasiolaumiwa. (Lakini) anayetaka kinyume cha haya basi hao ndio warukao mipaka (ya Allaah).” [Al-Mu-uminuwn: 5-7].
Kwa hiyo Aayah hizi zinatubainishia kwamba ndoa zinazoruhusiwa ni mke na wale iliyowamiliki mikono ya kuume, na kinyume na hawa basi ni haramu, hivyo mut’ah ni zinaa, tunamuomba Allaah Atukinge na shari.
Amesema Shaykh ´Abdullaah bin Jibriyn kwamba: “Raafidhwah katika kuhalalisha mut’ah wanaitumia Aayah iliyokuja katika Suratun Nisaa Aayah ya 24:
“Na pia (mmeharamishiwa) wanawake wenye (waume zao) isipokua wale iliyowamiliki mikono yenu ya kuume (ndio) shari’ah ya Allaah juu yenu. Na mmehalalishiwa (kuoa wanawake) wasio hawa muwatafute kwa mali zenu, kwa kuwaoa bila ya kufanya zinaa. Basi wale mnaowaoa miongoni mwao wapeni mahari yao yaliyolazimishwa. Wala si vibaya kwenu katika (kutoa) yale mliyoridhiana badala ya yale yaliyotajwa. Hakika Allaah ni mjuzi na mwenye hekima.” [An-Nisaa: 24].
Na jawabu la hoja hii ni kwamba: Hakika Aayah zote hizi kuanzia aayah ya 19 hadi aayah ya 23 zinazungumzia ndoa,
[Enyi mlioamini! Si halali kwenu kuwarithi wanawake kwa nguvu.] [An-Nisaa: 19].
[Na mkitaka kubadilisha mke mahali pa mke…] [An-Nisaa: 20]. Hadi kauli Yake:
[Wala msiwaoe wake waliowaoa baba zenu…] [An-Nisaa: 22]. Hadi kauli Yake:
[Mmeharimishiwa mama zenu…] [An-Nisaa: 23].
kisha baada ya kutaja wale walioharamishwa kwa nasabu na kwa sababu zingine Akasema Allaah:
[Mmehalalishiwa wanawake wengine wasiokuwa hawa waliotajwa…] [An-Nisaa: 24].
Maana yake, imehalalishwa ndoa kwa wanawake wote waliobaki, hivyo, mkiwaoa kwa ajili ya kustarehe nao (kuwaingilia), basi muwape mahari yao ambayo mmefaradhishiwa kwao.
Hivyo ndivyo walivyoifasiri Aayah hii kongamano la Maswahaba na waliokuja baada yao.”(4)
Hata Sheikh wa kundi lao hilo, Atw-Twuwsiy katika kitabu chake ‘TahdhiybulAhkaam’ ameitaja kwa ubaya ndoa ya Mut`ah, anasema: “Kama akiwa mwanamke anatoka katika nyumba ya watu watukufu basi haifai kumuoa katika ndoa ya mut`ah, kwa kuchelea aibu itakayoipata familia yake na udhalili utakaompata yeye.”(5)
Bali hali imefikia kwa hawa Raafidhwah wanahalalisha kumuendea mwanamke kinyume cha maumbile (nyuma). Yamekuja haya katika ‘AlIstibswaar’ kutoka kwa ´Aliy bin Al-Hakam amesema: “Nilimsikia Swafwaan anasema: Nilimuuliza Ar-Ridhwaa nikasema: Hakika mmoja katika wafuasi wako kanituma nikuulize jambo ambalo yeye kaogopa na kaona aibu kukuuliza, akasema: Ni lipi? Akasema: Je, inafaa mtu kumuingilia mke wake kinyume cha maumbile (nyuma)? Akasema: “Ndio inafaa.”(6) *
1) Tafsiyr Manhajis-Swaadiqiyn cha Mullaa Fut-hullaah Al-Kaashaaniy 2/495.
2) Man Laa yahdhwuruhul-Faqiyh cha Ibn Baabawayhi Al-Qummiy uk. 330.
3) Tafsiyr Manhajis-Swaadiqiyn cha Mullaa Fut’hullaah Al-Kaashaniy 2/492-493 66 Al-Furuu minal-Kaafiy cha Al-Kulayniyiy 5/451 na At-Tahdhib 2/188.
4) Ni katika maneno ya Shaykh Ibn Jibriyn na dalili nyingine ya kuharamisha mut`ah katika
Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Hadiyth ya Rabiy’u bin Saburah AlJuhaniy kwamba baba yake alimuhadithia kwamba alikuwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Enyi watu hakika mimi nilikuwa nimekuruhusuni kufanya Mut`ah, hakika Allaah Ameiharamisha mpaka siku ya Qiyaamah, yeyote atakayekuwa na mwanamke ambaye kamuoa ndoa ya Mut`ah basi na amuache, na wala asichukue chochote alichokuwa kampa.” [Muslim 1406].
5) Tahdhiybul-Ahkaam cha Atw-Twuwsiy 7/227.
6) Al-Istibswaar cha Atw-Twuwsiy 3/243
* MIONGONI MWA ITIKADI ZA MASHIA ‘Abdullaah Bin Muhammad As- Salafiy Uk / 29-30