0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

FADHLA ZA SIKU KUMI ZA MWEZI WA MFUNGO TATU

FADHLA ZA SIKU KUMI ZA MWEZI WA MFUNGO TATU

Mwenyezi Mungu Alipomuumba mwanadamu ili aje afanye ibada na Akaumba Pepo na Moto, kwa mwenye kutwii na mwenye kuasi. Akawawekea misimu ya ibada nyakati mbalimbali ili wazidishe thawabu waingie peponi kwa usahali.

Mwenyezi Mungu (Subhanahu wa Ta’aala) ameumba mbingu na Ardhi na akajichagulia mbingu ya saba na Ardhuni akachagua mji wa Makka pakawa ni patakatifu, akaumba pepo na Malaika, akaifanya firdausi ndio pepo ya juu zaidi, na Jibril ndiye kiongozi wa Malaika, na katika mwaka akaweka miezi, siku, nyakati za siku na saa. Akachagua mwezi mtukufu wa Ramadhani, na akachagua siku ya Ijumaa ndio siku bora, na akachagua usiku mtakatifu ni Lailatul Qadri, na saa ya kukubaliwa dua ipo Ijumaa, na akachagua masiku matukufu yapo kwenye siku kumi za mwanzo wa mfungo tatu. Allah akawaumba wanadamu, akawachagua aliowathamini ni muuminina, na akawachagua katika muuminina mitume, akawapandisha cheo mitume fulani, akaita rusul, na katika rusul akawapandisha wengine wanajulikana Ulul–‘azm, na katika hao akatubainishia vipenzi vyake, na bila shaka katika vipenzi vya Allah kiongozi wao ni Mtume wetu Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam).
Mu’min anaishi akiwa amebarikiwa
Muislamu alibarikiwa na Mwenyezi Mungu, aliwekewa madaftari mawili, moja kuandikiwa mazuri yake na jengine kuandikiwa mabaya yake. Ama kafiri aliwekewa daftari moja tu analoandikiwa mabaya tu. Ni juu ya Muislamu awe na lengo la kwenda peponi ajizatiti kiibada kila zama na awe na malengo kwa kila msimu, kwani Mola na Mtume walitueleza siri hiyo. Mungu(Subhaanahu wa Taala)amesema:

من جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا ۖ وَمَن جَاءَ بِالسَّيِّئَةِ فَلَا يُجْزَىٰ إِلَّا مِثْلَهَا وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ}   الأنعام:160}

[Afanyae wema atalipwa mfano wake mara kumi. na afanyae ubaya hatalipwa ila sawa nao tu. Na wao hawatadhulumiwa.]     [Al-An’aam:160]

Na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akaongezea:[Hata kama hakulifanya hilo jema lakini alitia nia pia atalipwa thawabu. Na aliyetia nia ya ubaya na akalifanya hilo ataandikiwa alifanya ubaya moja na Mwenyezi Mungu hamwangamizi ila atakayekuangamia].
Hivi ina maana ya kuwa twa-a ya Muislamu kwa Mola Muumba ina baraka kote kote, katika matamshi na vitendo vyake, ulimi wake umtaje Allah na kutaja mazuri mpaka kufa kwake, na yeye afanye mema mpaka awe na mwisho mwema. Maneno haya yametafsiriwa na swahaba, Maliki Ibn Swa’aswaa alikuwa akisema: “Vitendo vitano vya Muislamu, atalipwa malipo ya vitendo hamsini na saumu ya Ramadhani moja atalipwa miezi kumi, na siku sita za mwezi wa Shawwal, kila siku moja atalipwa siku kumi, kwa hivyo mwenye kufunga Ramadhani na siku sita za Shawwal ni kama aliyefunga mwaka.”
Ama sadaka, Mola atampa daraja mtoaji mpaka daraja mia saba. Na hijja isiyokuwa na makosa, malipo yake ni ya juu sana isipokuwa kustahiki Pepo. Twaa ni kisafisho cha kujisafishia dhambi, kama Mtume alivyofananisha swala na kuoga mara tano, jee atabakiwa na uchafu? Na kila ibada ina baraka zake.
Zama zenye Baraka zaidi kiibada ni Siku Kumi za Mfungo Tatu
Allah(Subhaanahu wa Taala) anavyotupendelea tupate thawabu zaidi, alitudokezea kuwa kuna siku kumi ambazo ni muhimu sana na akaziapia nazo, Akasema allah (Subhanahu wa Ta’aala):

وَالْفَجْرِ  وَلَيَالٍ عَشْرٍ}     الفجر:1-2}

[Naapa kwa alfajiri,Na kwa masiku kumi,]   [Al Fajr:1-2]

Na Allah huapia kwa viumbe vitukufu au nyakati tukufu, au Ardhi tukufu. Kama mbingu na Ardhi, Alfajiri na Alasiri, au Makkah au akaapa kwa chochote Alichoumba.

FADHLA ZA SIKU KUMI ZA FUNGO TATU

Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Alikutanisha ibada tukufu zaidi kwa wakati mtukufu zaidi, kwa mfano swalatul fajri na swalatul asri kwa nyakati zake ambapo wanakutana Malaika wa vipindi viwili na kuchanganikana na waumini, ndio Anaapa kwa Alfajiri na Anaapa kwa Alasiri. Mwenyezi Mungu Amezitukuza siku kumi hizi, ndani imo siku ya ‘Arafa, siku ya idd ya kuchinja na kadhalika. Na Amekutanisha swala ya usiku, na Yeye huteremka kila usiku, na Yeye amesema kwamba waja wema ni wale wanaoacha vitanda vyao wakaswali, kwa sababu ya kumuogopa Yeye, na kutaka pepo na mambo yao ya kilimwengu, Nami hapo usiku huwa nikiwauliza haja mbalimbali niwapatie, lakini kuna biri baina yao na shetani. Mmoja katika watu wema amesema: ‘Haikubakia ladha ya dunia isipokuwa swala ya usiku, na swala ya jamaa na kutangamana na watu wema’.
Ulikamilika uislamu katika siku kumi hizi, ambapo ndani yake kuna ibada mbalimbali na watu wakajitenga na maovu, ilivyokamilika Dini, ndio Sunna ikapata nguvu na bid’a ikavunjika. Allah (Subhaanahu wa Taala) Amesema:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا}    المائدة:3}

[Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini.]     [Al-Maaida:3]

Anasema Sahaba ‘Umar bin Khatwab: ‘Mimi naijua vizuri Aya hii ilipoteremka, iliteremshwa siku ya Arafa, siku ya Ijumaa, maswahaba wengi miongoni mwetu tukafahamu dini imekamilika na Mtume yuko safarini kuondoka’. Mmoja katika wanavyuoni wa kiyahudi anaelezea umuhimu wa siku hii na kuteremka kwa Aya hii nzito, “Lau kama ni dini ya kiyahudi, siku hii ingekuwa iddi ya kila mwaka.”
Kabla ya kuhuishwa tena uislamu, kulikuwepo na dini nyingi ambazo ziliwapeleka motoni kama vile ukiristo, uyahudi, umajusi na kadhalika. Lakini ulipohuishwa uislamu, dini zote ziliyayuka na uislamu ndio utakaobaki mpaka Qiyama, na siku hii ya ‘Arafa ndio neema ilipotimia na makafiri wakawa wamekatazwa wasiingie Makkah, Waislamu wakazidi kuwa kitu kimoja.
Kuna ibada zinazokusanyikana hapa, siku za hija, kuna swala, sadaka, kufunga sunna au kufunga kwa ambaye hakupata kuchinja, kuna dhikri na kadhalika mpaka imalizike hija.
Msimu wa ibada wa siku hizi kumi, haupatikani ila kwa mwaka mara moja. Dakika zake, saa, siku na wiki, ndizo zinazompendeza Mwenyezi Mungu, lau mwanadamu atajitahidi kiibada siku hizi, atakuwa amefaulu sana. Kwa hadithi iliyopokewa na Ibn ‘Abaas kuwa amesema bwana Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam):

ما من أيام العمل الصالح فيها أحب إلى الله من هذه الأيام ـ يعني أيام العشر ـ قالوا يا رسول الله ولا الجهاد في سبيل الله ؟ قال ولا الجهاد في سبيل الله إلا رجل خرج بنفسه وماله ثم لم يرجع من ذلك بشيء

[Hakuna siku bora kwa Mwenyezi Mungu anazolipa thawabu nyingi kama siku hizi kumi. Maswahaba wa Mtume wakamuuliza: hata kwenda jihadi?, Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akawajibu: Hata kwenda jihadi, isipokuwa aliyetoka jihadi na mali yake, akafa huko na mali yake asirudi na kitu]    [Imepokewa na Bukhari]

Ndio atakuwa ana thawabu nyingi kushinda huyu mwenye kufanya amali katika siku kumi
Katika siku hizi kumi, siku ya tisa inajulikana ni siku ya ‘Arafa, inajulikana kwa thawabu na msamaha mwingi kutoka kwa Allah, ndio siku waumini wanapeleka dua zao kwa wingi. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [Dua bora ni dua ya siku ya ‘Arafa].
Na kwa sababu waumini wengi wameacha machafu yao kwa ajili ya ‘Arafa, mahujaji na wasiokuwa mahujaji na ndio siku ya hijja kubwa. Na mwenye kufunga siku hii husamehewa madhambi ya mwaka uliopita na mwaka ujao.
Ipo siku ya mwisho, siku ya kumi ya mfungo tatu, inayojulikana kuwa ni siku ya kuchinja, zipo ibada tofauti tofauti, kutupa vijiwe, kunyoa, kutufu, kukimbia baina ya Swafaa na Marwaa, kuchinja na kuswali Iddi.
Fadhila za siku hii ni nyingi. Muislamu anatakikana asizipoteze, bali azipatilize na ashindane katika mambo ya kheri na ajishughulishe kwa amali njema.

SIKILIZA MADA HII NA SHEIKH YUSUF ABDI

Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.