AR-RAHEEQ AL-MAKHTUM
Tumetaja kuwa watu sita miongini mwa watu wa Yath’tib (Madina) walisilimu katika msimu wa Hijja mnamo mwaka wa kumi na moja wa Utume na waliweka ahadi kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (ﷺ) kuwa watafikisha ujumbe wake kwa jamaa zao Madina. Kutokana na ahadi hiyo msimu uliofuata wa mwaka wa kumi na mbili wa Utume, mnamo mwezi wa Julai mwaka wa 621 C.E, walikuja watu kumi na wawili miongoni mwao walikuwemo watu watano katika wale waliougana na Mtume wa Mwenyezi Mungu (ﷺ) mwaka uliotangulia, mtu wa sita ambaye hakuhudhuria ni Jabir bin Abdillah bin Riab. Watu saba wengine walikuwa ni:-
1. Muadh bin Al-Harith Ibni Afraa kutoka katika kabila la BanuAn-Najar Katika Khazraji).
2. Dhakwan bin Abdi Al-Qays kutoka Banu Zuraiq (katika Khazraji)
3. Ubada bin Swamiti, kutoka Banu Ghanani (katika Khazraji)
4. Yazidi bin Tha’alaba, katika marafiki wa Banu Ghanam (katika Khazraji)
5. Al Abbas bin ’Ubada bin Fadhlah katika Banu Salim, (katika Khazraji)
6. Abu Haytham bin Tayhani katika Banu Ash-hal (katika Ausi)
7. Uwaym bin Saidah kutoka Banu Amri bin Aufi (katika Ausi) wawili katika hao ni katika Ausi na waliobaki wote ni katika Khazraj’
Watu hawa wote waliungana na Mtume wa Mwenyezi Mungu (ﷺ) Aqabah huko Mina. Wakamwahidi Bay’atu An Nisaa, ni sawasawa na ile ahadi ya wanawake ambayo ilishuka wakati wa Fathu Makka.
Bukhari amepokea kutoka kwa ’Ubada bin Swamiti kuwa Mtume (ﷺ) alisema,
بَايِعُونِي علَى أنْ لا تُشْرِكُوا باللَّهِ شيئًا، ولَا تَسْرِقُوا، ولَا تَزْنُوا، ولَا تَقْتُلُوا أوْلَادَكُمْ، ولَا تَأْتُوا ببُهْتَانٍ تَفْتَرُونَهُ بيْنَ أيْدِيكُمْ وأَرْجُلِكُمْ، ولَا تَعْصُوا في مَعروفٍ، فمَن وفَى مِنكُم فأجْرُهُ علَى اللَّهِ، ومَن أصَابَ مِن ذلكَ شيئًا فَعُوقِبَ في الدُّنْيَا فَهو كَفَّارَةٌ له، ومَن أصَابَ مِن ذلكَ شيئًا ثُمَّ سَتَرَهُ اللَّهُ فَهو إلى اللَّهِ، إنْ شَاءَ عَفَا عنْه وإنْ شَاءَ عَاقَبَهُ فَبَايَعْنَاهُ علَى ذلكَ.
”Njooni, nipeni ahadi ya kuwa hamtakishirikisha kitu chochote na Mwenyezi Mungu (s.w.t), hamtaiba, hamtazini, hamtawaua watoto wenu na hamtauleta uzushi ambao mtauzua kati ya mikono yenu na miguu yenu na kuwa hamtaniasi katika maamrisho ya kutenda mema. Atakayetekeleza haya miongoni mwenu malipo yake yako kwa Allah (s.w.t) na atakayetenda jambo katika mambo hayo ataadhibiwa hapa duniani, kuadhibiwa huko kutakuwa ni kafara kwake na atakayetenda jambo katika mambo hayo na Mwenyezi Mungu (s.w.t) Akamsitiri, basi jumbo lake Mwenyezi Mungu Atalisitiri, Akitaka Atamuadhibu na Akitaka Atamsamehe. ” Akasema, ”Nikampa ahadi.” Na pahala pengine imesemwa, ”Tukula kiapo juu ya hilo. (1) .
BALOZI WA UISLAMU MADINA
Baada ya kutimia kiapo cha ahadi ya utii kwa Mtume (ﷺ) na msimu ukamalizika, Mtume (ﷺ) alimpeleka pamoja na hawa waumini walioweka ahadi Balozi wa kwanza huko Yathri’b. Pamoja na ‘kazi nyingine, awafundishe Waislamu Sheria za Kiislamu na awafahamishe Dini, pamoja na kusimama kueneza Uislamu kati ya wale ambao bado ni Washirikina. Aliyechaguliwa kuwa Balozi ni kijana katika vijana wa Kiislamu, Mus’ab bin ’Umair Al-Abdary (Radhi za Allah ziwe juu yake).
MAFANIKIO YANAYOFURAHISHA.
Mus’ab bin ‘Umair (Radhi za Allah ziwe juu yake) alifikia kwa Asiad bin Zurarah na kwa pamoja wakawa wanautangaza Uislamu kwa watu wa Yathrib kwa jitihada na hamasa. Mus’ab akapewa jina la Al- Muqriu (yaani msomeshaji wa Qur’an). Miongoni mwa mambo ya kufurahisha yaliyopokewa katika kufanikiwa kwa Mus’ab (Radhi za Allah ziwe juu yake) katika kazi yake ya Da’awa ni kuwa, siku moja alitoka na Asiad bin Zurarah kuelekea nyumba za Banu Abdil Ashhal na Banu Dhafar. Wakaingia katika moja ya bustani miongoni mwa mabustani ya Banu Dhafar wakakaa kando ya kisima kinachoitwa Biiru Maraq — Waislamu wengi walikusanyika hapo (wakati Sa’ad bin Muadh na Usaid bin Khudhair waliokuwa mabwana miongoni mwa jamaa zao katika Banu Abdi Ashhal bado ni Washirikina). Walipolisikia jambo hilo, Sa’ad alisema kumwambia Usaid, ”Nenda kwa hawa watu wawili ambao inaelekea kuwa wamekuja ili kuwafanya wapumbavu watu wetu na ukawakemee na kuwakataza wasifike nyumbani kwetu, maana Asad bin Zurarah ni mtoto wa mama yangu. mkubwa na laiti isingelikuwa hivyo, ningelikwenda kumzuia mwenyéwe.” Usaid akachukua sime yake, na akawafuata, Asad alipomwuona aliwambia Mus’ab (Radhi za Allah ziwe juu yake), “HIuyo ni kiongozi wa jamaa zako amekufuata, mwambie ukweli kuhusu Mwenyezi Mungu (s.w.t).” Mus’ab (Radhi za Allah ziwe juu yake) akasema, ”Iwapo atakaa nitamsemesha.” ‘Usaid akafika na huku akitoa matusi na kuhoji ni jambo gani lililowaleta kwetu? Kwa nini mnawafanya watu wetu kuwa ni wapumbavu, ondokeni kama mnahaja na nafsi zenu; Mus’ab (Radhi za Allah ziwe juu yake) akamwambia, ”Kwa nini usikae na kusikiliza ujumbe tulionao, kama utaridhika na jambo lolote utalikubali na kama utalichukia utaliacha na kufanya hivyo ndiyo uadilifu, akakubali, akaichomeka chini sime yake na kukaa.” Mus’ab (Radhi za Allah ziwe juu yake) akaanza kumuelezea kuhusu Uislamu na mwisho akamsomea Qur’ani.
Baada ya kuisikiliza alisema, “Ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwa hakika tuliujua usoni mwake Uislamu kabla hajasema kutokana na kumeremeta na kumemetuka kwake”; Kisha akasema, “Ni uzuri ulioje wa aya hizo na ubora wake?’ Aliuliza, ”]e, Mtu akitaka kuingia katika dini hii anafanyaje? Akaelezwa; ”Utaoga, na kuzitakasa nguo zako, kisha utashuhudia Shahada ya ukweli, kisha utasali rakaa mbili.” Akasimama, akaoga na kuzizitakasa nguo zake na akatamka Shahada na akasali rakaa mbili. Baada ya hapo akasema, “Kwa hakika nyuma yangu yupo mtu, mtu huyu akiwafuateni basi hatabaki nyuma mtu yeyote katika jamaa zake na hivi ninakwenda kumleta kwenu hivi sasa.” Akaichukua sime yake na akaenda kwa Sa’ad na akamkuta amekaa katika jumba lao la mikutano akiwa na jamaa zake. Sa’ad alipomuona akasema, “Ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu jamaa yenu anawajieni na uso tofauti na ule ambao alikwenda nao kutoka kwenu.” Usaid alisimama katikati ya Jumba la mikutano na kumuuliza Sa’ad, ”Umefanya nini?.” Akajibiwa; ”Nimesema na wale watu, lakini ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu sikuwakuta na ubaya wowote na kwa hakika niliwakataza, lakini wakasema, Tutafanya lile ambalo unalipenda, na kwa hakika nimeelezwa kuwa Banu Haritha wametoka kwenda kwa As’ad bin Zurarah, ili wakamuue – na hilo ni kwa sababu yeye ni mtoto wa mama yako mkubwa ili waivunje ahadi yako.” Sa’ad akasimama hali ya kuwa ameghadhibika kwa sababu ya lile aliloambiwa, akachukua sime yake na akatoka kuwafuata na alipowaona walivyotulizana Usaid alielewa kuwa kwa hakika hakuna vinginevyo isipokuwa alitakiwa awasikilize. Aliwasimamia huku akitoa matusi na kupaza sauti, ”Ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu ewe Aba Umama, laiti kama isingelikuwa kwa udugu tulionao usingelithubutu kulifanya jambo hili kwangu, katika majumba yetu na yale ambayo tunayachukia? Mus’ab (Radhi za Allah ziwe juu yake) akakumbuka maneno aliyoambiwa na As’ad kuwa, ”Huyu ni Bwana ambaye nyuma yake pana jamaa wengi, iwapo atakufuata hatabaki nyuma yoyote katika wao.” Akasema kumwambia Sa’ad bin Muadh, ”Hivi huwezii kukaa ili usikilize? Kama utaliridhia jambo utalikubali na iwapo utalichukia tutaliondoa lile ambalo unalichukia.” Akasema, ”Kwa hilo umefanya uadilifu”, akaichomeka chini sime yake na akakaa ili kusikiliza. Mus’ab (Radhi za Allah ziwe juu yake) akamfahamisha kuhusu Uislamu na mwisho akamsomea Qur’an, alisema, tukaujua katika uso wake Uislamu kabla hajatamka kutokana na kukunjuka kwake na kumeremeta kwake, na kisha akauliza, ”Huwa mmnafanya nini mtu anapotaka kusilimu? Wakamfahamisha; ”Utaoga na utazitakasa nguo zako, kisha utashuhudia Shahada ya kweli na baada ya hapo utasali rakaa mbili.” Akafanya kama alivyoelekezwa na baadaye akachukua sime yake na kurudi kwenye Jumba la Mikutano kwa jamaa zake, walipomwona tu walisema; ”Tunaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu amerudi na uso tofauti na ule ambao alikwenda nao.” Alipofika na kusimama mbele yao aliwauliza; “Enyi Banu Abdil Ashhal mimi mnanifahamu kwa sifa ipi kwenu?’ Wakamjibu, ”Wewe ni Bwana wetu na ni mbora wetu kwa maoni na mwema wetu zaidi kwa tabia.” Akasema; “Kwa hakika kuanzia sasa maneno ya wanaume wenu na wanawake wenu kwangu ni haramu mpaka mumwamini Mwenyezi Mungu (s.w.t) na Mtume wake (ﷺ).” Jua halikuchwa siku hiyo isipokuwa wote wanaume na wanawake miongoni mwao walikuwa tayari wamekwisha kuwa Waislamu, isipokuwa mtu mmoja aliyekuwa akiitwa Al- Uswairim huyu alichelewa kusilimu mpaka siku ya vita vya Uhud. Aliposilimu tu aliingia vitani na kuuawa, hakuwahi kumsujudia Mwenyezi Mungu (s.w.t) sijida yoyote, kuhusu mtu huyu Mtume (ﷺ) alisema, ”Ametenda kidogo na amelipwa sana. ”
Mus’ab (Radhi za Allah ziwe juu yake) alifanya makazi yake katika nyumba ya As’ad bin Zurarah, akiwalingania watu kwenye Uislamu. Haikubaki nyumba yoyote katika nyumba za Answari isipokuwa ndani yake mlikuwa na wanaume na wanawake ambao tayari walikuwa wamekwisha ingia katika Uislamu, isipokuwa nyumba ya Banu Umayyah bin Zaid, Khatma na Wail, ambao walikuwa wakikaa na Qais bin Aslat, mshairi waliyekuwa wakimtii ambaye aliwachelewesha kuingia katika Uislamu mpaka mwaka wa Khandaq, mwaka wa tano baada ya Hijra, kabla ya kuingia msimu wa Hijja iliyofuata. Katika mwaka wa kumi na tatu, Mus’ab bin Umair (Radhi za Allah ziwe juu yake) alirudi Makka kumpelekea Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) khabari njema za mafanikio na akamsimulia khabari za makabila ya Yathrib na vipaji mbalimbali vya kheri walivyonavyo na mambo mengine katika uwezo wa nguvu na misimamo thabiti.