AR-RAHEEQ AL-MAKHTUM
Mtume ﷺ alipokea amri nyingi kwa Kauli Zake Mwenyezi Mungu ﷻ:
{يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ قُمْ فَأَنذِرْ وَرَبَّكَ فَكَبِّرْ وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ وَالرُّجْزَ فَاهْجُرْ وَلَا تَمْنُن تَسْتَكْثِرُ وَلِرَبِّكَ فَاصْبِرْ}
[Ewe uUyejifunika maguo!, Simama uonye (viumbe). Na Mola wako umtukuze, Na nguo zako uzisafishe. Na mabaya yapuuze, (endelea kuyapuuza). Wala usiwafanyie ihsani (viumbe) ili upate kujikithirishia (wewe hapa duniani). Na kwa ajili ya Mola wako fanya subira (kwa kila yatakayokufika]. ” [74:1-7]
Haya ni maamrisho mepesi ya kawaida katika mtazamo wa nje, lakini yenye maana kubwa kabisa katika lengo lake, na yaliyo na nguvu katika athari zake kwa kuhamasisha vitendo katika uhakika wa mambo na uhalisi wake:
1. Kikomo cha kusimamia uonyaji ni kuwa asiachwe mtu yeyote katika wale wanaokhalifu amri na kwenda kinyume na yale yanayomridhisha Mwenyezi Mungu ﷻ katika ulimwengu huu wa viumbe, isipokuwa awe ameonywa na Adhabu Zake Allah ﷻ, nampaka utokee mtikisiko wa tetemeko katika moyo wake.
2. Lengo la Kumtukuza Mwenyezi Mungu ﷻ ni kuwa kusiwepo na mkubwa yeyote katika ardhi, isipokuwa ajue kuwa uwezo wake utavunjwa, utapinduliwa ‘nje ndani na kuangamizwa usibaki katika ardhi isipokuwa Ukubwa wa Mwenyezi Mungu Aliye Mtukufu.
3. Lengo la kuzisafisha nguo na kuyaepuka masanamu ni kutufikisha katika kusafisha sehemu ya nje na ya ndani. Kutufikisha pia katika kuitakasa nafsi na takataka zote na uchafu wote mpaka kufikia kiwango cha mwisho cha ukamilifu. Ukamilifu unaowezwa kufikiwa na nafsi ya mwanaadamu chini ya kivuli cha Rehema za Mwenyezi Mungu ﷻ Zilizokienea kila kitu, Hifadhi Yake, Ulinzi Wake, Mwongozo Wake na Nuru Yake. Mpaka awe ni mfano wa juu katika jamii ya wanaadamu, ili zivutike Kwake nyoyo zilizosalimika, na nyoyo zilizopotoka kuhisi Ukubwa Wake, mpaka idhihirike kwake dunia yote kwa kupatana au kutofautiana.
4. Lengo la kutotaka ziada kwa kutoa, ni kumuasa kuwa asivihesabu vitendo vyake na jitihada zake kuwa ni mambo makubwa sana. Lakini pia asiache kuwa anajitahidi katika kutenda mema, kufanya juhudi na kujitoa muhanga. Kisha ayasahau yote hayo na azingatie zaidi kupata Radhi za Mwenyezi Mungu ﷻ, kwa sifa ya kuwa hatayahisi yale ambayo ameyatoa na kuyafanya.
5. Katika aya ya mwisho, pana ishara kwenye yale ambayo yalimtokea, katika kumpinga, kumcheza shere, kumkejeli, kufanya juhudi za kutaka kumwua, kuwaua masahaba wake, pamoja na kutaka kuwaangamiza waumini waliotaka kujitinga naye. Mwenyezi Mungu ﷻ Alikuwa Akimwamrisha kusubiri kwa yote hayo, kwa uvumilivu na kwa ajili ya kupata radhi za Allah.
Mwenyezi Mungu ﷻ ni Mkubwa. Ni Wepesi ulioje wa maamrisho haya katika sura yake ya nje, na uzuri ulioje katika kuathiri kwake kulikotulizana kwenye kuvutia. Ubora na uzito ulioje katika utendaji wa kuzichambua pepo kali zenye kuvuma kwa kasi zinazokusanya pande zote za ulimwengu na kuziunganisha baadhi yake na baadhi. *
*Ar-Raheeq Al Makhtum 112-113