ALAMA ZA SIKU YA QIYAMA
Ni lazima kwa kila Muislam ajue nguzo za imani,na niliza kuamini nguzo kama hizo na kutenda amali njema kwa ajili yake. na Katika nguzo za imani kuna kuamini siku ya kiama ambayo ni siku ya mwisho siku ya malipo. na kabla siku hii haijafika kuna alama za kuonesha kwamba imeshakaribia. Na sio siri kwani zimesha dhihiri baadhi ya alama,kwa hivyo ni vyema muislamu ajiandae na siku hiyo,Mwenyezi Mungu ﷻ Anasem:
فَهَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا السَّاعَةَ أَن تَأْتِيَهُم بَغْتَةً ۖ فَقَدْ جَاءَ أَشْرَاطُهَا ۚ فَأَنَّىٰ لَهُمْ إِذَا جَاءَتْهُمْ ذِكْرَاهُمْ} محمد:18}
[Kwani wanangoja lingine ila kiama kiwajie? basi alama zake zimekwisha kuja, kutawafaa nini wakati kitakapowajia] [ Muhammad : 18].
Ni lazima kwa kila muislamu kuamini siku ya mwisho alipe umuhimu mkubwa suala hili, kwani haikamiliki imani ya mtu mpaka aamini alama za kiama (kwani kuamini alama hizo ni katika kuamini siku ya kiama)ukizingatia kwamba Mtume ﷺ alizitaja alama hizi na hakitasimama kiama mpaka zitokee alama hizi. Swahaba Hudhaifa ibn Asiid radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake amesema:[ Tulikuwa tumekaa katika kivuli cha chumba cha Mtume ﷺ tukataja kiama na sauti zetu zikawa juu (mpaka Mtume ﷺ akasikia) akasema :
[إنها لن تقوم حتى ترون قبلها عشر آيات]
[Hakika hakitosimama kiama mpaka muone kabla yake alama kumi]. [Imepokewa na Muslim].
Na Mwenyezi Mungu ﷻ Amebainisha ya kwamba siku ya kiama haijulikani ni wakati gani na wala hakuna anayejua isipokuwa yeye peke yake. Na hakumhusisha yoyote kukijuwa kiama si Malaika aliyekurubishwa wala Mtume aliyetumilizwa na Mwenyezi Mungu. Pia imebainishwa kwamba kiama kimekaribia wakati wake kama zilivyoeleza Aya za Quran Tukufu na hadithi za Bwana Mtume ﷺ Mwenyezi Mungu s.w. Amesema:
يَسْأَلُونَكَ عَنِ السَّاعَةِ أَيَّانَ مُرْسَاهَا ۖ قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ رَبِّي ۖ لَا يُجَلِّيهَا لِوَقْتِهَا إِلَّا هُوَ ۚ ثَقُلَتْ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ لَا تَأْتِيكُمْ إِلَّا بَغْتَةً ۗ يَسْأَلُونَكَ كَأَنَّكَ حَفِيٌّ عَنْهَا ۖ قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ اللَّهِ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ الأعراف:187
[Wanakuuliza kuhusu kiama kitakuja lini? sema: ilimu yake iko kwa Mola wangu tu hakuna wa kudhihirisha wakati wake ila yeye. Imekuwa nzito mbingu na ardhi, hakita kuja kiama ila ghafla] [Al-Araaf : 187].
Amesema Mwenyezi mungu Subhaanahu wa Taala :
{يَسْأَلُكَ النَّاسُ عَنِ السَّاعَةِ ۖ قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ اللَّهِ ۚ وَمَا يُدْرِيكَ لَعَلَّ السَّاعَةَ تَكُونُ قَرِيبًا} الأحزاب:63
[Watu wanakuuliza kuhusu kiama kitakuja lini? sema: ilimu yake iko kwa Mola wangu tu. Na kipi kitakacho kujulisha lini kiama, pengine kiama kiko karibu] [Al-Ahzab : 63].
Na pale Jibril alipomuuliza Mtume Swalla Llahu ‘alayhi wasallam kuhusu kiama Mtume ﷺ akajibu:
[hakuwa mwenye kuulizwa ni mjuzi kuliko anayeuliza]
Aya na hadithi za Mtume ﷺ zinazoshiria kwamba hakuna anayejuwa wakati wa kutokea kiama isipokuwa Mwenyezi Mungu ﷻ.
Vile vile mitume waliobakia hawajui wakati gani kiama kitasimama.
Kwa kweli Mwenyezi Mungu amebainisha wazi kwamba kiama kimekaribia na vile vile Mtume wetu Muhammad rehma na amani zimfikie ameweka wazi katika hadithi zake kwamba kiama kimekaribia sana.
Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Amesema kwenye Qurani Tukufu:
{وَمَا يُدْرِيكَ لَعَلَّ السَّاعَةَ تَكُونُ قَرِيبًا} الأحزاب:63
[Na kipi kitakujulisha lini kiama pengine kiko karibu] [Al-Ahzab : 63].
Mwenyezi mungu Subhaanahu wa Taala Amesema:
{اقْتَرَبَ لِلنَّاسِ حِسَابُهُمْ وَهُمْ فِي غَفْلَةٍ مُّعْرِضُونَ} الأنبياء:1
[imekaribia watu hisabu yao(ya kiama)nao wamo katika kughafilika na wanalipuuza] [Al-Anbiya : 1].
Mtume ﷺ Nasema:
[بُعِثْتُ أَنَا وَالسَّاعة هكذا – ويشير بأصبعيه فيمدُّ بهما] رواه البخاري ومسلم
[Nimetumilizwa na kiama kama vidole viwili]. Akashiria vidole viwili cha kati na cha shahada. [Imepokewa na Bukhari wa Muslim]
VIGAWANYO VYA ALAMA ZA QIYAMA
Kwa hakika alama za kiama zimegawanyika vigawanyo viwili.
Alama ndogo.
Alama kubwa.
Alama ndogo ni zinatangulia au zinazokuja kabla ya siku kiama kwa mda mrefu na zinazoeleka na zinaweza kudhihiri baadhi yake pamoja na alama kubwa au zikaja baada ya alama kubwa.
Ama alama kubwa ni mambo makubwa ambayo yatadhihiri karibu na kiama na huwa si ya kawaida kwa mfano kuja Dajjal na nyenginezo.
Na ukizingatia kudhihiri kwake zimegawanyika vigawanyo vitatu
Alama zilizodhihiri na kuweko
Alama zilizodhihiri na bado zinatokea
Alama ambazo hazijatokea mpaka sasa.
ALAMA NDOGO ZA SIKU YA QIYAMA
Alama ndogo za kiama nazo ni kama zifuatazo;
1. Kutumilizwa Mtume ﷺ.
Mtume ﷺ amesema:
[بُعِثْتُ أَنَا وَالسَّاعة هكذا – ويشير بأصبعيه فيمدُّ بهما] رواه البخاري ومسلم
[Nimetumilizwa na kiama kama vidole viwili]. Akashiria vidole viwili cha kati na cha shahada.
2. Kufa Mtume ﷺ ni miongoni mwa alama ndogo za kiama, kwani ni ishara wazi ya kukatika wahyi kutoka mbinguni.
3. kudhihiri fitna kubwa; itachanganyika haki na batili zitatikisika imani mpaka mtu ataamka asubuhi hali ya kuwa ni muislamu na atalala hali ya kuwa ni kafiri au atalala hali ya kuwa ni kafiri na ataamka hali ya kuwa ni muislamu.
Hii ni kuonesha kwamba mtu kuingia katika ukafiri ni wepesi kwa kule kuchanganyika haki na batili na ndio hali za zama zetu hizi, watu wamechanganyikiwa kiasi kwamba hawajui haki ni ipi na batili ni ipi. Na kila ikidhihiri fitna atasema haya ndio maangamivu yangu kisha itaondoka itakuja nyingine atasema muumini haya ndio maangamivu na na hazitawacha fitna kudhihiri kwa watu mpaka kiama kisimame. Mtume ﷺ amesema:
إن بين يدي الساعة فتنا كقطع الليل المظلم, يصبح الرجل فيها مؤمناً ويمسي كافراً, ويمسي مؤمناً ويصبح كافراً, القاعد فيها خير من القائم, والقائم فيها خير من الماشي, والماشي فيها خير من الساعي رواه أحمد وأبوداود وإبن ماجة
[Hakika kabla ya kiama kutakuwa na fitna kama kipande cha usiku wa giza mtu ataamka muislamu na atalala kafiri na atalala kafiri na ataamka muislamu na aliyekaa ni bora kuliko aliyesimama na aliyesimama ni bora kuliko aliyetembea na anayetembea ni bora ni kuliko anayekwenda mbio]. [Imepokewa na Ahmad na Abuu Dawud na Ibnu Maajah]
4.Kudhihiri moto katika ardhi ya Hijazi na kupotea amana. Mtume ﷺ:
[لا تقوم الساعة حتى تخرج نار من أرض الحجاز، يضيء لها أعناق الإبل ببُصرى] رواه البخاري ومسلم
[Hakitasimama kiama mpaka utoke moto katika ardhi ya Hijazi unatoa mwangaza moto huo kiasi utaona shingo za ngamia Basra]. [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
Hakika moto huu umeshadhihiri katikati ya karne ya saba mwaka 654 hijria na ulikuwa mkubwa waliweza kuuona wanavyuoni wengi ambao waliokuwa zama hizo na waliokuja baada yao katika kuuelezea moto huo.
5. Vilevile kupotea amana ni katika alama za kiama watu kutotekeleza majukumu waliopewa na kutowajibika inavyotakiwa, Mtume ﷺ asema:
[إِذَا ضُيِّعَتِ الأَمَانَةُ فَانْتَظِرِ السَّاعَةَ] رواه البخاري
[Ikipotea amana ngojea kiama]. [Imepokewa na Bukhari]
6. Kuenea zinaa kiasi kwamba litakuwa jambo la kawaida na asiyejihusisha na jambo hilo watu. Mtume ﷺ:
والذي نفسي بيده؛ لا تفنى هذه الأمة حتى يقوم الرجل إلى المرأة، فيفترشها في الطريق، فيكون خيارهم يومئذ من يقول لو واريتها وراء هذا الحائط أخرجه أبو يعلى في مسنده حديث وصححه الألباني في الصحيحة
[Naapa kwa ambae nafsi yangu iko mkononi mwake hautamalizika umma huu mpaka asimame mwanamume na mwanamke na amlaze njiani afanye nae zinaa aseme mbora wao siku hiyo lau mtazunguka nyuma ya ukuta (mufanyie huko) ]. [Imepokewa na Abuu Ya’alaa katika Musnadi yake na kusahihishwa na Al Baniy]
7. Kuenea ribaa tukijua kuwa riba ni katika madhambi makubwa sana lakini namna itakavyoenea litakuwa jambo la kawaida, lakini watu hawajali na watajaza matumbo yao haramu.
Mwenyezi mungu Subhaanahu wa Taala Amesema:
{وَأَحَلَّ اللَّهُ الْبَيْعَ وَحَرَّمَ الرِّبَا ۚ} البقرة:275}
[Na Mwenyezi Mungu amehalalisha biashara na ameharamisha riba ] [Al-Baqara : 275].
Mtume ﷺ amesema:
[بين يدي الساعة يظهر الربا، والزنا، والخمر] رواه الطبراني
[Kabla ya kuja kiama kutadhiri riba na zinaa na pombe]. [Imepokewa na Al Twabraniy]
8. Kudhihiri na kuenea muziki kwa wingi na watu watahalalisha miziki hiyo, Mtume ameeleza haya katika hadithi zake nyingi suala hili kwa hivyo inatakiwa Waislamu wachunge mipaka ya Mwenyezi Mungu kwa kuomba msamaha kwake na kutubia, kwani hali za wanaadamu ni mbaya na za kusikitisha sana. Huku tusisahau kupeana nasaha kwa kuamrishana mema na kukatazana yalio mabaya.
9. Watu kujenga majumba makubwa na marefu tena kutoka kwa watu walio kuwa duni katika jamii kufikia kiwango cha utajiri na haya ni kwa mujibu wa maneno ya Mtume ﷺ:
[أن تلد الأمة ربتها، وأن ترى الحفاة العراة العالة رعاء الشاء يتطاولون في البنيان] رواه البخاري
[Ni kuzaa mtumwa wa kike bwana wake na utaona watu wasiokuwa na viatu waliouchi, masikini, wachunga mbuzi wanashidana kurefusha majumba]. [Imepokewa na Bukhari]
Na Mtume ﷺ Amesema:
[لَا تَقُومُ السَّاعَةُ حَتَّى يَتَبَاهَى النَّاسُ فِي الْمَسَاجِدِ] رواه أبوداود وصححه الألباني
[Hakitasimama kiama mpaka watu wajifakhiri kwa kujenga Misikiti]. [Imepokewa na Abuu Dawud na kusahihishwa na Al Baaniy]
10.Kukithiri uongo baina ya watu, watadanganyana kwa wingi huku tunajua kwamba uongo ni katika makosa makubwa Aliyoyakataza Mwenyezi Mungu katika Qurani na vile vile Mtume rehma na amani zimfikie ameukataza uongo katia hadithi zake tukufu. Mtume ﷺ amesema katika hadithi yake:
[لا تقوم الساعة حتى تظهر الفتن ، ويكثر الكذب ، وتتقارب الأسواق] رواه مسلم
[Hakitasimama kiama mpaka zidhihiri fitna, kukithiri uongo na kukaribiana masoko]. [Imepokewa na Muslim]
11. Vilevile hakitasimama kiama mpaka atamani aliye hai mauti kwa namna hali za watu zitakavyokuwa mbaya. Mtume ﷺ:
[لا تقوم الساعة حتى يمر الرجل بقبر الرجل ، فيقول : يا ليتني مكانه] رواه البخاري ومسلم
[Hakitasimama kiama mpaka mtu aende kwa kaburi la mtu aseme natamani mahali pako]. yaani atatamani alie hai afe yeye. [Imepokewa na Bukhari na mMusli]
Kukaribiana masoko ni miongoni mwa dalili za kiama kama ilivyo tanguli katika Hadithi.
[Hakitasimama kiama mpaka kukithiri uongo na kukaribiana masoko].
Hizi ndio miongoni mwa alama chache za kiama na ni vyema kwa muislamu yoyote azijue vizuri kwani akiziona huenda akajiandaa na siku ya mwisho kabla hajafikiwa na mauti kwa kufanya vitendo vizuri na kujiepusha na vitendo vibaya.
SIKILIZA MADA HII NA SHEIKH HASSAN SUGO