0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

UADUI WA ABUU LAHAB NA CHUKI YAKE DHIDI YA MTUME ﷺ

AR-RAHEEQ AL-MAKHTUM


Katika baadhi ya mapokezi inasimuliwa kuwa, wakati alipokuwa juu ya mlima wa Swafaa – alichukua jiwe ili ampige nalo Mtume  

Abu Lahab alikuwa amewaozesha watoto wake wawili, Utba na Utaybah, mabinti wawili wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu , Ruqayya na Ummu Kulthuum, kabla ya kupewa Utume. Baada ya kupewa Utume aliwaamrisha watoto wake kuwaacha kwa nguvu na mabavu; matakwa yake yalitekelezwa, na wakaachika. (1)
Wakati Abdullah mtoto wa pili wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu alipofariki, Abu Lahab alifurahia sana, na akaendaharaka haraka kwa marafiki zake kuwapasha khabari alizoziita njema; kuwa Muhammad amekuwa hana ukoo wenye kuendelea. (2)

Tumekwisha kueleza kuwa Abu Lahab alikuwa akizunguka nyuma ya Mtume ﷺ katika msimu wa Hijja na katika masoko kwa ajili ya kumkadhibisha.

Twariq bin Abdillahi Al-Muhariby amepokea maneno ambayo yanafahamisha kuwa Abu Lahab alikuwa haishii katika kuadhibu tu, lakini alikuwa akimpiga kwa mawe mpaka vikatoa damu visigino vyake. (3)
Mke wa Abu Lahab, Ummu Jamil binti Harb bin Umayyah, dada wa Abu Sufyan, alikuwa sawa na mume wake katika kumfanyia uadui Mtume ﷺ. Yeye alikuwa akichuma miba na kuiweka mlangoni kwa Mtume ﷺ wakati wa usiku. Alikuwa ni mwanamke wa maneno mengi, aliyekuwa na matusi na aliyechonga ulimi wake kwa kuzua na kumsingizia Mtume ﷺ mambo ya uzushi na kuwasha moto wa fitina. Aliendesha kampeni ya uovu dhidi ya Mjumbe wa Mwenyezi Mungu ﷺ na kwa sababu hiyo Qur’ ani ilimtaja kuwa ni mbebaji wa kuni. 
Siku alipoyasikia yale ambayo yalishuka kumhusu yeye na mume wake ndani ya Qur’an, alimfuata Mjumbe wa Mwenyezi Mungu ﷺ wakati amekaa msikitini mbele ya Al-Ka’aba, akiwa pamoja na Abubakar Al-Siddiq (r.a), akiwa amebeba jiwe lililokuwa na ukubwa wa kujaa kitanga, aliloliokota kutoka katika lundo la mawe huko nje. Alipoingia ndani ya msikiti alimwona Abubakar (r.a) ameketi, akamfuata nakumwuliza, ‘Yuko wapi rafiki yako?’ Mwenyezi Mungu ﷻ Alikuwa Ameyachukua macho yake Kuyaepusha na Mjumbe wake ﷺ, kwa hiyo akawa hamuoni; isipokuwa alimwona Abubakar (r.a) peke yake. Akasema, “Ewe Abubakar zimenifikia khabari kuwa ananitukana, Ninaapa kwa Jina la Mwenyezi Mungu laiti ningelimkuta hapa ningeupiga mdomo wake kwa jiwe hili. Ninaapa kwa Jina la Mwenyezi Mungu , hakika hata mimi ni mshairi.’ Kisha akasema: “Mwenye sifa mbaya tumemuasi, jambo lake tumelikataa, na dini yake tumeichukia.” 

Baada ya kumaliza beti zake akaondoka kwa hasira, Abubakar (r.a) akamwuliza Mtume ; “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu imekuwaje, kwani hakukuona?” Mtume   akamjibu: “Ndio hakuniona, kwa hakika Mwenyezi Mungu  aliyachukua macho yake.” (4)
Al-Bazzar amekipokea kisa hiki, na katika upokezi wake ni kuwa wakati Ummu Jamil aliposimama . kumsimamia Abubakar (r.a) na rafiki yake. alisema, ‘Ewe, Abubakar rafiki yako ametutukana’, Abubakar (r.a) akasema, ‘Hapana, Ninaapa kwa Mola wa jengo hili, yeye si mtunga mashairi wala si mwimbaji wa hayo mashairi.” Ummu Jamil akasema, “Hakika wewe ni mwenye kuaminiwa.”   

Abu Lahab aliyafanya yote hayo na hali yeye ni Ibni ammi wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu na jirani yake katika makazi yao. Nyumba yake ilikuwa imeambatana na nyumba ya Mtume (s.a.w) kama ambavyo walikuwa watu wengine katika majirani za Mjumbe wa Mwenyezi Mungu  walivyokuwa wakimuudhi na hali ya kuwa yuko nyumbani kwake. 


(1) 146 Fy Dhilalil Qur’an

(2) 147 Tafhimul Qur’an, Juzuu 6, Uk. 490.

(3) Ttirmidhy

(4) Sira lbn His/tarn, Juzuu I, Uk. 335-336.

* Arraheeq Al Makhtum Uk, 145-147


Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.